Wito huo umetolewa na mkuu wa kikosi cha usalama barabarani Mohamed
Mpinga wakati wa uzinduzi wa kampeni mpya ya kuhamasisha usalama
barabarani ijulikanayo zuia ajali sasa,toa taarifa mapema ambayo
inafanywa na kituo cha ITV na Radio One kwa kushirikiana na Vodacom
pamoja na jeshi la polisi, ambapo amesema matukio ya ajali yatapungua
endapo madereva wote watazingatia kanuni na sheria za usalama
barabarani.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika kituo kikuu cha mabasi
Ubungo jijini Dar es Salaam mkurugenzi wa Radio One Sterio Deogratius
Rweyunga amesema lengo la kituo cha ITV na Radio One ni kuhakikisha
madereva hasa wanaobeba abiria na kwenda masafa marefu wanakuwa makini
wawapo barabarani na kutii sheria ili kunusuru maisha ya watu na kutaja
namba za kutoa taarifa za mienendo mibaya ya madereva ambayo ni
0800757575.
Baadhi ya madereva wa mabasi ya mikoani wameeleza sababu kadhaa
zinazochangia ajali za barabarani ikiwemo ubovu wa miundombinu pamoja na
abiria wenyewe ambao wamekuwa wakiwachochea kuongeza mwendo kwa madai
ya kucheleweshwa wanakokwenda huku wakitishia kuhama kampuni ya basi
husika kutokana na dereva kwenda mwendo mdogo.
No comments:
Post a Comment