Mhasibu wa Hospitali ya Rufaa KCMC, Paul Mhumba amesimamishwa
kazi kwa tuhuma za kutuma ujumbe wa simu ya mkononi (sms) kwa Rais
Jakaya Kikwete.
Kuvuja kwa ujumbe huo na nambari ya simu
iliyotuma, kumeibua hisia tofauti kuhusu usiri wa ofisi ya Rais katika
kushughulikia malalamiko nyeti ya wananchi na kuwaweka njiapanda watoa
habari za siri.
Mhumba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha
Wafanyakazi wa Afya na Serikali Kuu (Tughe) Tawi la KCMC anadaiwa na
Menejimenti ya KCMC kuwa ndiye aliyetuma ujumbe huo.
Katika barua yake ya Mei 5, yenye kumbukumbu PF.4515/22, KCMC ilidai uchunguzi umebaini kuwa Mhumba ndiye mtumaji wa ujumbe huo.
“Uongozi umepokea taarifa iliyotumwa mwishoni mwa
Aprili na mwanzoni mwa Mei mwaka huu kwa njia ya ujumbe wa simu kwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Jakaya Kikwete,” ilidai.
KCMC imedai katika barua hiyo, taarifa hiyo ya sms
ilibeba ujumbe unaohusiana na matumizi mabaya ya fedha za hospitali
hiyo unaofanywa na baadhi ya viongozi na Shirika la Msamaria Mwema
(GSF).
Mbali na tuhuma hizo, lakini pia KCMC inadai
taarifa hiyo ilimweleza Rais kuwa KCMC na GSF linalomiliki hospitali
hiyo, zinajitosheleza kwa mapato, hivyo hakuna haja kwa Serikali
kuendelea kuipatia ruzuku.
Pia, menejimenti imedai taarifa hiyo ilidai
wafanyakazi wa KCMC wanatumikishwa kama watumwa, hivyo ni maombi yao
(watumishi) Serikali ilegeze masharti ili ajira zao zichukuliwe na
Serikali.
“Uchunguzi umeonyesha kuwa taarifa hiyo (kwa
Rais), umeituma kwa kutumia simu ya kiganjani ambayo ulikabidhiwa kama
mojawapo ya zana ya kuleta ufanisi katika majukumu yako,” imedai.
Mei 8, KCMC ilimwandikia barua Mhumba yenye
kumbukumbu PF.4515/28 iliyotiwa saini na Profesa Raimos Olomi
ikimjulisha kuwa amesimamishwa kazi kuanzia Mei 8 hadi Mei 14.
Katika barua hiyo, Profesa Olomi alidai
menejimenti imepokea taarifa ya kutofanyika kwa kikao cha kamati ya
nidhamu baada ya Mhumba kumkataa mwenyekiti kutokana na kukosa imani
naye.
Pia, kikao hicho hakikufanyika baada ya Mhumba
kuomba kamati hiyo iahirishwe kwa sababu mwakilishi wake hakuwapo na
kikao kingine kupangwa Mei 15.
Hata hivyo, bado mhasibu huyo hajarejeshwa kazini na vikao
vilikuwa vinaendelea kuhusu hatua za kinidhamu zinazostahili dhidi yake.
“Wakati hayo mambo mawili yanafanyiwa kazi,
menejimenti imeamua kukusimamisha kazi. Kabla hujaondoka unatakiwa
ukabidhi vitendea kazi pamoja na simu ya mkononi uliyokabidhiwa,”
imedai.
Ofisa Uhusiano wa KCMC, Gabriel Chisseo alipoulizwa kuhusu sakata hilo alisema kwa nafasi yake, hawezi kulizungumzia.
Mhumba alipotafutwa wiki iliyopita, alikiri
kusimamishwa kazi kwa tuhuma za kumtumia Rais ujumbe wa simu ya mkononi,
ingawa alikanusha kuhusika.
“Maudhui hayo kama ni kweli yalitumwa, hayana
matatizo. Nimeongea na katibu mkuu kumuuliza kama alipokea sms kutoka
kwa Rais na kuwapa KCMC na namba ya mtumaji amekanusha,” alidai.
Hata hivyo, alidai yeye akiwa mwenyekiti wa Tughe,
amekuwa akionekana kama adui pale anapojaribu kutetea masilahi ya
watumishi, likiwamo suala la kutopandishwa daraja tangu mwaka 2007 hadi
2015.
“Ni kweli, watumishi hawajapandishwa madaraja
tangu 2007. Sisi (Tughe) tumekuwa tukilipigania kwa sababu linachangia
wastaafu kulipwa pensheni ndogo,” alisema.
“Mimi kama kiongozi wa wafanyakazi, niko tayari
kupeleka ushahidi kwa mambo ambayo Tughe tumekuwa tukipambana nayo,
ikiwamo mahali zilipo fedha za mashine ya CT-Scan,” alisema Mhumba.
Tawi la Tughe KCMC, limemwandikia barua katibu
mkuu wa Tughe, ikiomba Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama
aingilie kati suala hilo ili haki itendeke.
Gama alipoulizwa kuhusu suala hilo, alikiri kupigiwa simu na Mhumba akimueleza lakini alimshauri aziandikie mamlaka husika.
Gama alisema akiwa mwakilishi wa Rais mkoani
Kilimanjaro, atachunguza nini kimetokea baada ya kupata malalamiko rasmi
kutoka kwa Mhumba au Tughe yenyewe.
CHANZO; MWANANCHI
CHANZO; MWANANCHI
No comments:
Post a Comment