Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Augustino
Mrema amesema hakuna ubaya Rais Jakaya Kikwete akiachwa kuongeza nchi
kwa muda ili akamilishe mchakato wa Katiba Inayopendekezwa pamoja na
Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Hivi karibuni viongozi wanaounda Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa), walidai kuwa Serikali na Tume ya Uchaguzi (NEC)
inachelewesha uboreshaji wa Daftari la Wapigakura kwa lengo la kutaka
kumwongezea Rais Kikwete muda wa kukaa Ikulu.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema ni
miezi mitatu imebaki kabla ya kampeni za uchaguzi, lakini mpaka sasa
ratiba, majimbo yaliyogawanywa, watumishi wala vituo vya uchaguzi bado
haviwekwa bayana na wala haifahamiki kazi ya uandikishaji katika Daftari
la Wapigakura halijakamilika katika mikoa miwili.
“Hiyo ni hatari sana kwa Taifa. Tunaionya NEC
isijaribu kufanya mbinu zitakazosababisha kuahirishwa kwa Uchaguzi Mkuu
wa Oktoba mwaka huu,” alisema Mbowe.
Akizungumza jana, Mrema alisema yeye
ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kutoa wazo la kutaka Rais Kikwete
aongezewe muda zaidi wa kukaa Ikulu kwa kuwa kuna mambo mengi ambayo ni
ya muhimu kwa Taifa yanayotakiwa kukamilika kabla ya Uchaguzi Mkuu.
Mrema alisema alitoa maoni hayo mwaka jana wakati
viongozi wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) walipokutana na Rais
Kikwete mjini Dodoma, lakini alishangaa kuona viongozi wengine wakipinga
wazo hilo.
“Nilitoa ushauri Rais Kikwete akiwepo. Nilisema
tusogeze Uchaguzi Mkuu mbele kwa miaka miwili ili atuachie nchi ikiwa
salama, lakini wapinzani wamejiandaa kuingia Ikulu waliniona mimi kama
bundi,” alisema Mrema.
Aliongeza kuwa hata Rais Kikwete hakuonekana
kufurahishwa na hali hiyo iliyojitokeza baada ya kauli yake na kwamba,
hivi sasa amebaini kuwa kiongozi huyo wa nchi hataki kuongezewa hata
siku moja ya kuendelea kukaa Ikulu.
“Sema kwa sababu wenzangu wamejiandaa kuingia
Ikulu mwaka huu, wameshawaandaa hata wake zao kuwa ‘ma-first lady’,
lakini ukweli ni kwamba hata Katiba Inayopendekezwa ikipitishwa lazima
kuwe na muda wa mpito.
“Simfanyii mtu kampeni, ninachosema ni kwamba,
mambo hayajakamilika na tunataka yakamilike na michakato yote
aliyeianzisha ni Rais Kikwete, ni vyema akaimaliza,” alisema Mrema.
Akihutubia kwenye sherehe ya maadhimisho ya Siku
ya Wafanyakazi Duniani jijini Mwanza juzi, Rais Kikwete alisema hana
mpango wa kuongeza muda kama baadhi ya wanasiasa wanavyodai.
“Nawashangaa wanaodai kuwa Serikali ina mpango wa
kuongeza muda wa urais, sina mpango wa kufanya hivyo, tarehe imepangwa
na uchaguzi utafanyika kwa mujibu wa Katiba,” alisema Rais Kikwete.
No comments:
Post a Comment