Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu jana
alichafua hali ya hewa bungeni baada ya kudai kuwa Serikali ya Awamu ya
Nne ni ya kichovu, kauli ambayo ilizua mabishano makali kati yake na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista
Mhagama.
Akichangia Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu 2015/16,
Lissu alisema Serikali hiyo imeshindwa karibu kila jambo, ikiwamo
uandikishaji wa wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Alisema uchovu huo pia umejidhihirisha wazi baada
ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kueleza kwamba mpaka sasa haijapewa
fedha za maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, wakati imebaki miezi
mitano ufanyike.
Lissu alivutana na Spika Anne Makinda pale
alipotakiwa kukaa chini kumpisha Mhagama azungumze baada ya kugoma kwa
maelezo kuwa waziri huyo ameingilia wakati akitoa ufafanuzi wa uchovu wa
Serikali.
Mvutano huo ulianza Lissu alipokuwa akisema kuwa
mbali na kukwama kwa uandikishaji katika Daftari la Wapigakura, hata
katika upigaji wa kura za kupitisha Katiba Inayopendekezwa katika Bunge
Maalumu la Katiba, marehemu, mahujaji na wagonjwa ni miongoni mwa
wajumbe wa Bunge hilo waliopiga kura.
“Hata Uchaguzi Mkuu mpaka sasa Serikali haijatoa
fedha kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, hakuna maandalizi yoyote.
Hatukubali kuona Serikali hii ikijiongezea muda kwa kisingizio hicho,”
alisema Lissu.
Kauli hiyo ilimwinua Mhagama na kueleza kuwa
katika Bunge la Katiba zilipigwa kura halali, huku akifafanua jinsi
Serikali ilivyofanya shughuli nyingi za maendeleo.
“Mheshimiwa Spika, Lissu analidanganya Bunge.
Kauli zake ni za kuudhi namwomba asiendee kupotosha umma,” alisema
Mhagama huku Lissu akisisitiza kauli yake.
Wakati Mhagama akisimama kuomba utaratibu wa
Spika, Lissu naye alisimama akipinga kitengo cha kukatizwa na waziri
huyo kuchangia, tukio ambalo liliingiliwa na Spika na kuzua majibizano.
“Huyu ananizuia kwa misingi gani, kafuata
utaratibu upi,” alisema Lissu huku Mgahama naye akiendelea kuzungumza
huu akiwa amesimama kabla ya wote wawili kukatishwa na Spika Makinda
aliyewataka wakae chini na kufafanua kuwa yeye ndiye anayejua utaratibu.
Baada ya kutoa ufafanuzi huo, Makinda alimpa
nafasi Mhagama kuendelea kuzungumza na alipomaliza alimpa nafasi Lissu
ili amalizie kuchangia hotuba hiyo.
Mbowe
Awali, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman
Mbowe aliwasilisha hotuba ya kambi hiyo, akisema hakuna maandalizi
yoyote yanayofanywa na Serikali ambayo yanaashiria wazi kuwa Uchaguzi
Mkuu utafanyika Oktoba mwaka huu.
Mbowe ambaye pia hakumaliza kusoma hotuba yake
baada ya kukatishwa na Spika wa Bunge, Makinda baada ya kuibuka ubishi
juu ya muda wa uwasilishaji, alisema hayo wakati akitoa maoni ya kambi
ya upinzani kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Alisema ukweli huo umethibitishwa na NEC kwenye
ukurasa wa randama ya Tume hiyo namba 13 unaosema: “Kwa upande wa
maandalizi ya Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu, 2015 Tume hatujapokea
fedha hadi sasa.”
Alihoji kama Serikali haijaipatia Tume fedha kwa
ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu, inategemea miujiza gani kuwa
ifikapo Oktoba uchaguzi huo utafanyika.
“Ni lini zabuni zitatangazwa kwa ajili ya
makandarasi mbalimbali ambao watasambaza vifaa kwa ajili ya Uchaguzi
Mkuu na tarehe ya kuwapata hao wazabuni ni lini?” alihoji.
Alisema wakati Serikali ikishindwa kuipatia NEC
fedha kwa ajili ya kufanya maandalizi ya uchaguzi ili ufanyike katika
mazingira ya amani, haki na utulivu, imeamua kuwekeza na kujiandaa
kupambana na wananchi wake.
“Hii ni kutokana na ukweli kuwa tuna taarifa kuwa
Serikali imeamua kuagiza zaidi ya magari 777 kwa ajili ya Jeshi la
Polisi, kuanzia yale ya maji ya kuwasha, doria na shughuli za ukaguzi
katika mwaka huu wa fedha,” alisema.
Alisema NEC inadaiwa madeni na makandarasi ambao
walisambaza vifaa kwenye uchaguzi uliopita ambayo yanathibitishwa kwenye
randama ukurasa wa 13, lakini hazikutengwa kwenye bajeti
Kura ya maoni
Mbowe alisema Sheria ya Kura ya Maoni ya Mwaka
2013, iliweka bayana muda maalumu wa kuchapisha swali la kura ya maoni,
kutoa elimu kwa umma na siku ya kufanyika kwa kura ya maoni na kuwa muda
wa kufanya yote hayo kwa mujibu wa sheria umeshapita.
“Haiwezekani tena kwa kura ya maoni kufanyika sasa
au baadaye bila kwanza sheria ya kura ya maoni ya mwaka 2013 kuletwa
bungeni.”
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment