Mkazi mmoja wa Kijiji cha Nanja, Kata ya Lepruko, wilayani
Monduli, anadaiwa kumuuza mtoto wake wa kumzaa kwa mtu mwingine kwa
Sh70,000 kwa madai kuwa ana maisha magumu.
Katika tukio hilo la kushangaza, inadaiwa mwanamke
huyo (jina linahifadhiwa) aliamua kumuuza mtoto huyo wa kiume mwenye
umri wa miezi minane katikati ya Mei, mwaka huu akiwa ametoka naye
mkoani Singida.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nanja, Time Samsoni
akizungumza juzi mbele ya Mratibu wa Chama cha Wanawake Wanasheria
Tanzania (Tawla) Tawi la Arusha, Francisca Gaspar alisema walijaribu
kumshawishi akamchukue mtoto wake, lakini aligoma.
Mwenyekiti Samsoni alidai kuwa mtu aliyemnunua
mtoto huyo anaishi katika Kijiji cha Longonito na ana wadhifa mkubwa
kijijini hapo.
“Kwa kweli tulisikitishwa na kitendo hicho cha
huyo mwanamke kumuuza mtoto wake kwa Sh 70,000 akisingizia maisha magumu
na ameshindwa kumlea,” alisema Samsoni.
Alisema walimwita mwanamke huyo kwenye ofisi ya
kitongoji na kumhoji sababu zilizomfanya amuuze mwanaye, lakini
aliwaaambia kuwa hana uwezo wa kumhudumia.
Mratibu wa Tawla, Gaspar alisema watahakikisha
wanafuatilia suala hilo ili lipatiwe mwafaka. “Lakini tumeambiwa kuwa
mama huyo ametoroka baada ya kuhojiwa na viongozi wa hapa kijijini na
hajulikani aliko mpaka sasa.”
Alisema katika kipindi hiki ambacho Tawla
inaadhimisha miaka 25 tangu ianzishwe, wanatoa elimu ya sheria kwa
wanawake wa eneo la Nanja na Meserani, hivyo jamii iwe inatoa taarifa
kwao wanapoona matukio kama hayo.
Nina uhakika kuna matukio mengi yanatokea huku
vijijini ila taarifa zinashindwa kufikishwa na endapo mngetuarifu
mapema, tungeshirikiana na polisi huyo mama aliyemuuza mtoto wake
angekamatwa kabla ya kutoroka,” alisema Gaspar.
Mkazi mmoja wa eneo hilo, James Lengitambi
alipongeza hatua ya mwanamke huyo kumuuza mtoto wake kuliko angemtupa
chooni au kwenye mfuko wa Rambo kama wanavyofanya wanawake wengine.
“Tumezoea kusikia kwenye vyombo vya habari kuwa
baadhi ya wanawake wanawatupa chooni watoto wao au kuwatelekeza kwenye
mifuko ya plastiki, ila huyu amemuuza hajamuua,” alisema Lengitambi
No comments:
Post a Comment