B.B King anayejulikana kama Riley B. King kwa jina la asili, alizaliwa mwaka 1925 katika jimbo la Mississippi nchini Marekani.
Baadaye akajitosa katika tasnia ya muziki mwaka 1940 na kushirikiana na wanamuziki maarufu kama vile Eric Clapton na U2 na kuweza kuburudisha kwenye tamasha zaidi ya 100 zilizoandaliwa kila mwaka.
Mkongwe huyo wa gita aliyefariki akiwa na miaka 89, aliwahi kulazwa hospitalini hivi karibuni kutokana na maradhi ya kisukari.
B.B King aliyewahi kushinda tuzo za Grammy mara 15, aliuza mamilioni ya albamu zake zinazojumuisha nyimbo maarufu kama vile "Lucille", "Sweet Black Angel" na "Rock Me Baby" zilizoshikilia chati.
Katika jarida la Rolling Stone lililochapishwa mwaka 2011, B.B King alishikilia nafasi ya 6 katika orodha ya wapigaji gita 100 bora duniani. Mnamo mwaka 2003, alikuwa akishikilia nafasi ya 3 katika orodha hiyo.
Mnamo mwaka 2005, bunge la jimbo la Mississippi alikozaliwa B.B King, lilitangaza kusherehekewa kwa siku maalum ya msanii huyo kwa heshima yake.
Wiki iliyopita tarehe 12 Mei, mji wa Memphis pia ukatangaza Siku ya B.B King.
Kigogo huyo wa muziki aliyetoa burudani na kupendwa na wengi, atakumbukwa na kuenziwa na wapenzi wa nyimbo za Blues.
No comments:
Post a Comment