Thursday, 21 May 2015

Wanafunzi wa chuo cha mifugo Tengeru wagoma kuingia madarasani

Wanafunzi  wa chuo cha mifugo Tengeru wamegoma kuingia madarasani kwa madai ya kutoridhishwa na utaratibu mzima wa uendeshwaji wa chuo chini ya wakala aliyekabidhiwa jukumu la kuendesha chuo hicho ambacho awali kilikuwa taasisi ya serikali.
Madai makubwa ya wanafunzi hao ni utaratibu wa utoaji wa vyeti vya taaluma wanayochukua  ambavyo wanadai havikidhi viwango pamoja na muda wa masomo.
Wanafunzi hao pia wanasema kilichosababisha kuchukua hatua ya kugoma ni kitendo cha mkurugenzi wa chuo hicho kukataa kukutana nao ili kuwaptia  ufafanuzi wa madai yao,hali ambayo rais wa serikali ya wanafunzi hao Elisamehe Mduma anasema imewalazimu kumuandikia barua katibu mkuu wizara ya maendeleo ya mifugo na kwamba mgomo huo hautakoma mpaka pale atakapofika kuwasikiliza.
Hata hivyo jitihada za kuupata uongoz wa chuo kuzungumzia madai hayo ya wanafunzi ziligonga ukuta baada ya wakufunzi waliokuwepo kudai kuwa mzungumzaji pekee ni mkurugenzi wa chuo ambaye amedaiwa kuwa safarini.

No comments: