Thursday, 28 May 2015

Ukawa wamshika pabaya Dk. Magufuli

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ‘umemshika pabaya’ Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kutokana na ukubwa wa deni linalodaiwa na wakandarasi.
Deni hilo limesababisha wabunge kutaka ufafanuzi wa kina kuhusu deni ambalo linazidi bajeti ya miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
Akiwasilisha Maoni ya Kambi ya Upinzani bungeni jana, Msemaji wa Upinzani katika wizara hiyo, Felix Mkosamali alimtaka Dk. Mgufuli kulifafanulia Bunge madeni ambayo yamefikia Sh bilioni 800.
Alisema katika mwaka wa fedha 2015/16, wizara hiyo imetenga bajeti ya maendeleo Sh bilioni 890.57 kwa taasisi zilizo chini yake wakati deni ni Sh bilioni 800.
“Mheshimiwa Spika, licha ya wizara hii kuwa na kelele na mbwembwe nyingi ukweli ni kwamba madeni ya wizara yanazidi fedha za maendeleo tunazopitisha katika Bunge lako tukufu,” alisema Mkosamali.
Mkosamali ambaye pia ni Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), alitoa mfano kuwa bajeti ya 2014/15, wizara ilikuwa na madeni yanayofikia Sh bilioni 760 huku bajeti ya maendeleo kwa wizara na taasisi zake zikiwa Sh bilioni 762.
Alisema huo ni ushahidi wizara hiyo haikuwa na fedha za maendeleo kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Kivuko Dar-Bagamoyo
Kuhusu kivuko cha Bagamoyo, Mkosamali aliliomba Bunge kuunda tume huru ya kuchunguza ununuzi wa kivuko hicho kwa sababu ni kibovu, licha ya kununuliwa kwa bei kubwa.
“Mheshimiwa Spika, ni jambo la ajabu kivuko hiki kimenunuliwa kwa takribani Sh bilioni nane, kinabeba abiria 300 kinatumia saa tatu kutoka Dar es Salaam kwenda Bagamoyo na kurudi mara moja tu kwa siku.
“Hali hii imechangia kivuko hiki kukosa abiria na hivyo wananchi wanaona afadhali kupanda daladala kuliko kivuko kinachotumia saa tatu.
Alisema kambi yake imebaini Dk. Magufuli amekuwa akiaandaa bajeti ndefu kuwachanganya wabunge huku akiunganisha barabara zilizojengwa miaka 1980 na 1990 kama vile zimejengwa leo.
KAPUYA
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati Miundombinu, Profesa Juma Kapuya alisema wakati wanachambua utekelezaji wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka2014/15 na makadirio ya 2015/16, walijulishwa kuwapo madeni makubwa ya wakandarasi na wahandisi washauri wa barabara ambayo yamekuwa yakiongezeka.
“Mheshimiwa Spika, kuendelea kulimbikiza madeni haya kunasababisha hasara mbalimbali kwa Serikali ikiwamo ongezeko la riba, kazi kufanyika kwa muda mrefu na wakandarasi wadogo kufilisika,”alisema Profesa Kapuya.
Trillioni 4/- Dar
Awali akiwasilisha bungeni mpango wa makadirio ya mapato na matumizi wizara yake kwa mwaka 2015/16, Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli alisema aliisema miradi yote iliyopangwa kutekelezwa na wizara yake itakapokamilika itagharimu Sh trilioni 4.394.
Waziri alisema sehemu ya barabara ya Dar es Salaam –Chalinze imepangwa kujengwa kwa kiwango cha barabara sita na itatekelezwa kwa utaratibu wa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP).
“Mheshimiwa Spika, suala la kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam ni suala mtambuka linalohusisha wizara na mamlaka mbalimbali zikiwamo halmashauri za Jiji.
“Maandalizi ya ujenzi barabara ya njia sita ya Dar es Salaam – Chalinze – Morogoro (kilomita 200) sehemu ya Dar es Salaam – Chalinze (kilomomita 100) imepangwa kujengwa kwa kiwango cha “Expressway”. Maandalizi ya mradi huu utakaotekelezwa kwa utaratibu wa ubia baina ya Serikali na Sekta Binafsi (Public Private Partnership – PPP) yameanza.
Kuhusu ujenzi wa daraja jipya la Selander, Dk. Magufuli alisema lengo kuu ni kupunguza msongamano wa magari katika eneo la Selander na Serikali ya Korea Kusini imekubali kuipatia Tanzania mkopo wa masharti nafuu kwa ajili ya ujenzi huo.
Alisema daraja hilo pamoja na barabara zake za maingilio litakuwa na urefu wa kilomita 7.2 na litaanzia eneo la Koko Beach kupitia Kenyatta Drive na kuingia baharini na kisha kuungana na barabara ya Barack Obama eneo la Hospitali ya Aghakan na utagharimu Sh bilioni 197.5.
Magufuli alisema katika kipindi cha miaka 10 Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, imejenga barabara zenye urefu wa zaidi ya kilomita 17,762.
Wabunge
Baadhi ya wabunge wameshangazwa na hatua ya Serikali kutenga bajeti ya Wizara ya Ujenzi isiyo halisi huku wengine wakipatwa na wasiwasi iwapo miradi mipya ya barabara itatekelezwa mwaka huu.
Katika michango yao bungeni jana, wabunge hao walisema wizara hiyo imezidiwa na madeni ya wakandarasi kutokana na Serikali kushindwa kutoa fedha na nyingine kutumiwa vibaya.
Mbatia
Akichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alisema bajeti hiyo ni kiini macho kutokana na kuzongwa na madeni makubwa ya wakandarasi.
“Wizara hii inadaiwa na wakandarasi deni la Sh bilioni 850 hadi bilioni 900 kuliko fedha zinazoombwa, hivi nyinyi mtafanyaje kazi kwa bajeti hii?
“Mwaka jana mfuko wa barabara ulitengewa Sh bilioni 600, lakini fedha hukupewa zote… Serikali hapa imevunja Katiba, ibara ya 135 inaeleza kuwa fedha zinazotengwa kwa kazi fulani zinapaswa kutumika kwa kazi husika.
“Wapo wakandarasi wanne wamepoteza maisha kutokana na kutolipwa madeni yao, hivi kweli hadi imefikia mahali wananchi wetu wanapoteza maisha kwa sababu ya madeni ya Serikali,” alisema.
Msigwa
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) alisema mkoani Iringa pekee wakandarasi wanaidai Serikali mabilioni ya shilingi jambo ambalo limeathiri hadi maisha ya mama lishe.
“Mimi nashangaa, sisi wabunge tunakwenda nje ya nchi tunaona barabara za wenzetu. Hizi barabara za wenzetu ni sawa na hizi za kwetu? Mbona tunajitoa fahamu, tuache kujikombakomba kwa vitu visivyokuwa na maana.
“Dar es Salaam ni jiji la mfano lakini miaka 30 imepita jiji halina master plan (mipango miji), eti wabunge wengine wanalinganisha barabara zetu na zile za Dubai, jamani tuache hizo.
“Hizi barabara zetu ni za kwenda migombani, huwezi kulinganisha barabara hizi na zile tunazoziona katika nchi za wenzetu, huwezi kujisifia kwa barabara ambazo ni disposable (za muda),” alisema.
Msigwa aliishangaa Serikali kununua Kivuko cha Bagamoto Dar es Salaam kwa gharama kubwa huku kikijiendesha kwa hasara.
“Kwa kivuko hiki mtu anaweza kwenda Zanzibar kutoka Dar es Salaam na kurudi mtu aliyetoka Bagamoyo hajafika Dar es Salaam. Kivuko kinatumia saa tatu nauli Sh 1500 kwa safari moja Serikali inapata Sh 450, 000 wakati mafuta yanayotumika katika kivuko hicho ni Sh milioni 2.4 waziri mnafanya kitu gani?” alihoji.
Mkosamali
Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), aliwashangaa wabunge wanaosifia Serikali badala ya kutimiza wajibu wao wa kuisimamia Serikali.
“Kuna mbunge mmoja alisimama hapa akaisifia Serikali, yaani fedha zinapunguzwa halafu mbunge anakuja hapa anasifia. Mwaka jana Serikali iliahidi kutoa Sh bilioni 10 Kigoma katika bajeti hii fedha iliyotengwa ni Sh bilioni 7, mtu anasifia,”alisema.
Sendeka
Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), alisema anawashangaa wabunge ambao wanaishambulia Serikali kutokana na bajeti ndogo badala ya kushauri namna ya kupata fedha.
“Kule kwangu Simanjiro hakuna hata hatua moja ya lami, acha kilomita moja, hatua moja hakuna lakini hii haiondoi ukweli kwamba Serikali imejitahidi katika sekta ya ujenzi.
“Zipo changamoto, madeni ni mengi, fedha haziendi hivi mnategemea Maguli atafanya kitu gani? Barabara haziwezi kujengwa kwa kupiga kelele tuunganishe nguvu sote kwa umoja watu,” alisema.
Mtemvu
Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu (CCM), alisema haungi mkono bajeti hiyo kutokana na tatizo la msongamano katika jiji la Dar es Salaam.
“Wananchi wa Temeke wamenituma nisiunge mkono bajeti hii na sababu ni moja tu, msongamano katika jiji la Dar es Salaam, hali ni mbaya, inatisha inatia huruma.
“Leo hii Dar es Salaam mtu anatumia saa sita kutoka kazini kwenda nyumbani kwake. Mheshimiwa Magufuli juzi ulisema asilimia 65 ya mapato inatoka Dar es Salaam, lakini hutuwatendei haki watu wa Dar es Salaam.
“Nakuomba mheshimiwa muda uliobaki ni mfupi tunaomba sana tusaidie tupate fedha kwa ajili ya barabara za ringroad (barabara za pete). Barabara nyingi Dar es Salaam hivi sasa hazipitiki kutokana na mvua na wakandarasi wamelipwa,” alisema.

No comments: