|
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (kulia) akifurahia jambo na wajumbe
wa Kamati Kuu ya chama hicho walipohudhuria kikao cha dharura katika
Hoteli ya Bahari Beach, jijini Dar es Salaam jana. kuanzia kushoto ni
Ezekia Wenje, Mchungaji Peter Msigwa na Naibu Katibu wa chama hicho
(Zanzibar), Salum Mwalimu. |
Licha ya Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF)
kupokea taarifa ya Ukawa na kuamua chama hicho kiendelee kushiriki
katika umoja huo, bado suala la mgombea urais wa vyama vinavyounda umoja
huo limeendelea kuwa siri nzito.
Taarifa
zilizopatikana kutoka ndani ya CUF jana, zilisema kuwa katika kikao
chake kilichoketi juzi na jana mjini Zanzibar, baraza hilo lilipokea
taarifa ya Ukawa, kuithibitisha na kuamua chama hicho kiendelee na
ushirikiano huo.
Mkutano wa waandishi wafutwa
Pamoja
na hayo, jana kutwa nzima viongozi wa Ukawa walikuwa kwenye vikao
mfululizo na hakukuwa na taarifa rasmi zilizopatikana na hata mkutano na
waandishi wa habari ulioitishwa jana jioni uliahirishwa bila kueleza
utaitishwa tena lini.
Ingawa taarifa ya mkutano wa
Ukawa na wanahabari haikutaja ajenda, habari zilizoenea katika mitandao
ya kijamii zilibainisha kuwa walikuwa wanakusudia ama kutangaza chama
kilichopitishwa na Ukawa kusimamisha mgombea urais au kutangaza jina la
mgombea mwenyewe pamoja na mgombea mwenza.
Vyanzo
mbalimbali ndani ya Ukawa, vilieleza kuwa ufunguo wa hatua hiyo ulikuwa
unashikiliwa na CUF, ambayo hivi karibuni ilijitenga na umoja huo ili
masuala yake yajadiliwe kwanza na vikao vyake vya maamuzi kabla ya
kurejea kwenye meza ya majadiliano.
Taarifa za uhakika
kutoka katika kikao hicho kilichoketi Zanzibar kwa siku mbili,
zilibainisha kuwa wajumbe waliafikiana kinyume na ilivyotarajiwa kuwa
wangevurugana.
Miongoni mwa mambo ambayo inadaiwa wameafikiana ni kuwa mgombea urais atoke Chadema na chama hicho kitoe mgombea mwenza.
Jussa: Watanzania mtafurahi
Hata
hivyo, mmoja wa wajumbe wa baraza hilo, Jussa Ismail Ladhu alipoulizwa
alisema ikiwa itaamuliwa mgombea mwenza wa Ukawa atoke CUF, hakutakuwa
na shida kwa kuwa chama hicho kina wanasiasa wazuri, safi na makini na
kwamba kitatoa mtu ambaye Watanzania wote watafurahi.
“Ikiamuliwa
kuwa mgombea mwenza atoke CUF, wananchi msiwe na wasiwasi, CUF ina
hazina nyingi, itatoa mtu bora, itawapa chaguo ambalo Watanzania wote
wataridhika nalo,” alisema Jussa.
Pamoja na
kuthibitisha kuwa Baraza hilo limeamua CUF iendelee kushiriki katika
umoja huo, Jussa alisema kwenye mjadala matatizo kidogo yalikuwapo
katika mgawanyo wa majimbo.
Hata hivyo alisema baada ya
kuweka vigezo vya kuwa na mgombea wa Ukawa, sasa hakuna shida kwa kuwa
majimbo machache yaliyosalia utaratibu wake utatangazwa hivi karibuni.
Kuhusu
mgombea mwenza, Jussa alisema CUF ina nafasi kubwa ya kutoa mgombea
huyo kwa sababu ndicho chama chenye nguvu Zanzibar na kina wanasiasa
mahiri na makini.
Wagombea wetu tunataka wawe ni wale
watakaohakikisha kuwa Katiba Mpya inapatikana mara baada ya uchaguzi ili
kuyaweka sawa mambo yanayohitaji kuwekwa sawa.
Hata
hivyo, kwa mujibu wa Katiba, mgombea urais na mgombea mwenza wanapaswa
kutoka chama kimoja, hivyo kama Chadema itamtoa mgombea urais inabidi
pia mgombea mwenza atoke chama hicho.
Habari ambazo bado si rasmi zinasema kuwa mmoja wa viongozi wa CUF anaweza kuhamia Chadema ili kukidhi matakwa hayo ya Katiba.
Mkurugenzi
wa Haki za Binadamu, Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF,
Salim Bimani alisema kuwa mambo katika Ukawa ni mazuri, wapo waliofikiri
kuwa watavurugana, lakini wamekubaliana na sasa Watanzania wasubiri
kupata wagombea safi katika ngazi zote.
Bimani alisema CUF kitaendelea kushirikiana na vyama vingine vya upinzani nchini ili kuhakikisha demokrasia inazidi kukua.