UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ‘umemshika pabaya’ Waziri wa
Ujenzi, Dk. John Magufuli kutokana na ukubwa wa deni linalodaiwa na
wakandarasi.
Deni hilo limesababisha wabunge kutaka ufafanuzi wa kina kuhusu deni
ambalo linazidi bajeti ya miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha
2015/2016.
Akiwasilisha Maoni ya Kambi ya Upinzani bungeni jana, Msemaji wa
Upinzani katika wizara hiyo, Felix Mkosamali alimtaka Dk. Mgufuli
kulifafanulia Bunge madeni ambayo yamefikia Sh bilioni 800.
Alisema katika mwaka wa fedha 2015/16, wizara hiyo imetenga bajeti ya
maendeleo Sh bilioni 890.57 kwa taasisi zilizo chini yake wakati deni
ni Sh bilioni 800.
“Mheshimiwa Spika, licha ya wizara hii kuwa na kelele na mbwembwe
nyingi ukweli ni kwamba madeni ya wizara yanazidi fedha za maendeleo
tunazopitisha katika Bunge lako tukufu,” alisema Mkosamali.
Mkosamali ambaye pia ni Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), alitoa
mfano kuwa bajeti ya 2014/15, wizara ilikuwa na madeni yanayofikia Sh
bilioni 760 huku bajeti ya maendeleo kwa wizara na taasisi zake zikiwa
Sh bilioni 762.
Alisema huo ni ushahidi wizara hiyo haikuwa na fedha za maendeleo kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Kivuko Dar-Bagamoyo
Kuhusu kivuko cha Bagamoyo, Mkosamali aliliomba Bunge kuunda tume
huru ya kuchunguza ununuzi wa kivuko hicho kwa sababu ni kibovu, licha
ya kununuliwa kwa bei kubwa.
“Mheshimiwa Spika, ni jambo la ajabu kivuko hiki kimenunuliwa kwa
takribani Sh bilioni nane, kinabeba abiria 300 kinatumia saa tatu kutoka
Dar es Salaam kwenda Bagamoyo na kurudi mara moja tu kwa siku.
“Hali hii imechangia kivuko hiki kukosa abiria na hivyo wananchi
wanaona afadhali kupanda daladala kuliko kivuko kinachotumia saa tatu.
Alisema kambi yake imebaini Dk. Magufuli amekuwa akiaandaa bajeti
ndefu kuwachanganya wabunge huku akiunganisha barabara zilizojengwa
miaka 1980 na 1990 kama vile zimejengwa leo.
KAPUYA
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati Miundombinu, Profesa Juma Kapuya
alisema wakati wanachambua utekelezaji wa bajeti ya wizara hiyo kwa
mwaka2014/15 na makadirio ya 2015/16, walijulishwa kuwapo madeni makubwa
ya wakandarasi na wahandisi washauri wa barabara ambayo yamekuwa
yakiongezeka.
“Mheshimiwa Spika, kuendelea kulimbikiza madeni haya kunasababisha
hasara mbalimbali kwa Serikali ikiwamo ongezeko la riba, kazi kufanyika
kwa muda mrefu na wakandarasi wadogo kufilisika,”alisema Profesa Kapuya.
Trillioni 4/- Dar
Awali akiwasilisha bungeni mpango wa makadirio ya mapato na matumizi
wizara yake kwa mwaka 2015/16, Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli
alisema aliisema miradi yote iliyopangwa kutekelezwa na wizara yake
itakapokamilika itagharimu Sh trilioni 4.394.
Waziri alisema sehemu ya barabara ya Dar es Salaam –Chalinze
imepangwa kujengwa kwa kiwango cha barabara sita na itatekelezwa kwa
utaratibu wa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP).
“Mheshimiwa Spika, suala la kupunguza msongamano wa magari katika
Jiji la Dar es Salaam ni suala mtambuka linalohusisha wizara na mamlaka
mbalimbali zikiwamo halmashauri za Jiji.
“Maandalizi ya ujenzi barabara ya njia sita ya Dar es Salaam –
Chalinze – Morogoro (kilomita 200) sehemu ya Dar es Salaam – Chalinze
(kilomomita 100) imepangwa kujengwa kwa kiwango cha “Expressway”.
Maandalizi ya mradi huu utakaotekelezwa kwa utaratibu wa ubia baina ya
Serikali na Sekta Binafsi (Public Private Partnership – PPP) yameanza.
Kuhusu ujenzi wa daraja jipya la Selander, Dk. Magufuli alisema lengo
kuu ni kupunguza msongamano wa magari katika eneo la Selander na
Serikali ya Korea Kusini imekubali kuipatia Tanzania mkopo wa masharti
nafuu kwa ajili ya ujenzi huo.
Alisema daraja hilo pamoja na barabara zake za maingilio litakuwa na
urefu wa kilomita 7.2 na litaanzia eneo la Koko Beach kupitia Kenyatta
Drive na kuingia baharini na kisha kuungana na barabara ya Barack Obama
eneo la Hospitali ya Aghakan na utagharimu Sh bilioni 197.5.
Magufuli alisema katika kipindi cha miaka 10 Serikali ya awamu ya nne
chini ya Rais Jakaya Kikwete, imejenga barabara zenye urefu wa zaidi ya
kilomita 17,762.
Wabunge
Baadhi ya wabunge wameshangazwa na hatua ya Serikali kutenga bajeti
ya Wizara ya Ujenzi isiyo halisi huku wengine wakipatwa na wasiwasi
iwapo miradi mipya ya barabara itatekelezwa mwaka huu.
Katika michango yao bungeni jana, wabunge hao walisema wizara hiyo
imezidiwa na madeni ya wakandarasi kutokana na Serikali kushindwa kutoa
fedha na nyingine kutumiwa vibaya.
Mbatia
Akichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia
(NCCR-Mageuzi), alisema bajeti hiyo ni kiini macho kutokana na kuzongwa
na madeni makubwa ya wakandarasi.
“Wizara hii inadaiwa na wakandarasi deni la Sh bilioni 850 hadi
bilioni 900 kuliko fedha zinazoombwa, hivi nyinyi mtafanyaje kazi kwa
bajeti hii?
“Mwaka jana mfuko wa barabara ulitengewa Sh bilioni 600, lakini fedha
hukupewa zote… Serikali hapa imevunja Katiba, ibara ya 135 inaeleza
kuwa fedha zinazotengwa kwa kazi fulani zinapaswa kutumika kwa kazi
husika.
“Wapo wakandarasi wanne wamepoteza maisha kutokana na kutolipwa
madeni yao, hivi kweli hadi imefikia mahali wananchi wetu wanapoteza
maisha kwa sababu ya madeni ya Serikali,” alisema.
Msigwa
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) alisema
mkoani Iringa pekee wakandarasi wanaidai Serikali mabilioni ya shilingi
jambo ambalo limeathiri hadi maisha ya mama lishe.
“Mimi nashangaa, sisi wabunge tunakwenda nje ya nchi tunaona barabara
za wenzetu. Hizi barabara za wenzetu ni sawa na hizi za kwetu? Mbona
tunajitoa fahamu, tuache kujikombakomba kwa vitu visivyokuwa na maana.
“Dar es Salaam ni jiji la mfano lakini miaka 30 imepita jiji halina
master plan (mipango miji), eti wabunge wengine wanalinganisha barabara
zetu na zile za Dubai, jamani tuache hizo.
“Hizi barabara zetu ni za kwenda migombani, huwezi kulinganisha
barabara hizi na zile tunazoziona katika nchi za wenzetu, huwezi
kujisifia kwa barabara ambazo ni disposable (za muda),” alisema.
Msigwa aliishangaa Serikali kununua Kivuko cha Bagamoto Dar es Salaam kwa gharama kubwa huku kikijiendesha kwa hasara.
“Kwa kivuko hiki mtu anaweza kwenda Zanzibar kutoka Dar es Salaam na
kurudi mtu aliyetoka Bagamoyo hajafika Dar es Salaam. Kivuko kinatumia
saa tatu nauli Sh 1500 kwa safari moja Serikali inapata Sh 450, 000
wakati mafuta yanayotumika katika kivuko hicho ni Sh milioni 2.4 waziri
mnafanya kitu gani?” alihoji.
Mkosamali
Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), aliwashangaa wabunge
wanaosifia Serikali badala ya kutimiza wajibu wao wa kuisimamia
Serikali.
“Kuna mbunge mmoja alisimama hapa akaisifia Serikali, yaani fedha
zinapunguzwa halafu mbunge anakuja hapa anasifia. Mwaka jana Serikali
iliahidi kutoa Sh bilioni 10 Kigoma katika bajeti hii fedha iliyotengwa
ni Sh bilioni 7, mtu anasifia,”alisema.
Sendeka
Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), alisema
anawashangaa wabunge ambao wanaishambulia Serikali kutokana na bajeti
ndogo badala ya kushauri namna ya kupata fedha.
“Kule kwangu Simanjiro hakuna hata hatua moja ya lami, acha kilomita
moja, hatua moja hakuna lakini hii haiondoi ukweli kwamba Serikali
imejitahidi katika sekta ya ujenzi.
“Zipo changamoto, madeni ni mengi, fedha haziendi hivi mnategemea
Maguli atafanya kitu gani? Barabara haziwezi kujengwa kwa kupiga kelele
tuunganishe nguvu sote kwa umoja watu,” alisema.
Mtemvu
Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu (CCM), alisema haungi mkono bajeti
hiyo kutokana na tatizo la msongamano katika jiji la Dar es Salaam.
“Wananchi wa Temeke wamenituma nisiunge mkono bajeti hii na sababu ni
moja tu, msongamano katika jiji la Dar es Salaam, hali ni mbaya,
inatisha inatia huruma.
“Leo hii Dar es Salaam mtu anatumia saa sita kutoka kazini kwenda
nyumbani kwake. Mheshimiwa Magufuli juzi ulisema asilimia 65 ya mapato
inatoka Dar es Salaam, lakini hutuwatendei haki watu wa Dar es Salaam.
“Nakuomba mheshimiwa muda uliobaki ni mfupi tunaomba sana tusaidie
tupate fedha kwa ajili ya barabara za ringroad (barabara za pete).
Barabara nyingi Dar es Salaam hivi sasa hazipitiki kutokana na mvua na
wakandarasi wamelipwa,” alisema.