WABUNGE
jana waligeuza Ukumbi wa Bunge sehemu ya mnyukano baada ya baadhi yao
kushambuliana, huku wakituhumiana kwa wizi na wamehongwa na uongozi wa
Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Independent Power Tanzania Limited
(IPTL).
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) na Mbunge wa Kigoma Kusini,
David Kafulila (NCCR-Mageuzi), jana waliwasha moto na kuibana serikali
kutaka iunde Tume Maalumu kuchunguza kashfa ya ufisadi wa zaidi ya sh
bilioni 200 zilizohifadhiwa kwenye akaunti ya Escrow ndani ya Benki Kuu
(BoT).
Mbali ya kutaka Bunge liunde Kamati Teule kuchunguza ufisadi huo,
wabunge hao kwa nyakati tofauti walitaka serikali ichunguze kifo cha
aliyekuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa, kwani wakati fedha
hizo zinakwapuliwa, waziri huyo alikuwa Afrika Kusini akiugua na
alishakata kauli.
Msimamo wa wabunge hao, uliungwa mkono na Mbunge wa Chama cha
Mapinduzi (CCM), Christopher Ole Sendeka, ambaye alilitaka Bunge kuunda
Kamati Teule kubaini ukweli wa kashfa hiyo.
Wabunge kwa nyakati tofauti waliwasha moto huo jana bungeni wakati wa
mjadala wa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa
Fedha 2014/2015.
Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Msemaji Mkuu
wa Kambi hiyo, Mnyika, alisema kuwa wezi wa fedha za Escrow wako ndani
ya Bunge hilo na maelezo yoyote kuwa taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) ifanye uchunguzi haitaungwa mkono na kambi ya upinzani
kutokana na historia yake.
Huku akiungwa mkono na wabunge wote wa kambi ya upinzani, alisema
Takukuru iliwahi kutumika kusafisha sakata la Richmond, hivyo hawana
imani kama inaweza kuja na matokeo ya uchunguzi sahihi ya kashfa hiyo.
Alisema Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa (CAG), nayo ilihusika
kumsafisha aliyekuwa Katibu Mkuu David Jairo, katika kashfa ya kugawa
fedha kwa wabunge ili waiunge mkono na kupitisha Bajeti ya Wizara hiyo
kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Akaunti hii ilifunguliwa ili fedha ambazo Tanesco ilipaswa kuilipa
IPTL kwa ajili ya tozo za uwekezaji ‘Capacity Charge’ ziwekwe hadi pale
mgogoro huo utakapomalizika.
Mnyika, alisema kwa mujibu wa taarifa ya Gavana wa Benki Kuu, Benno
Ndullu, aliyotoa katika kikao cha Kamati ya Uchumi ya Bunge
kilichofanyika Bagamoyo, alikiri kuwa alibanwa na viongozi wa juu kiasi
cha kushindwa kufurukuta.
Alisisitiza kuwa kauli za viongozi waandamizi wa serikali na Shirika
la Umeme nchini kwa nyakati tofauti kuhusu sakata hilo, zimezidisha
utata na kuchochea dhamira ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutaka
iundwe Kamati Teule ya Bunge kuchunguza.
Mnyika alihitimisha hoja yake kwa kukumbusha kwa mujibu wa Mtume
Muhamad (SAW) aliyesema kuwa mnafiki ni mtu mwenye nyuso mbili, ndani
yake na nje yake ni tofauti na alama zake ni tatu: akizungumza husema
uongo, akiahidi hatimizi na akiaminika hufanya hiyana.
“Mheshimiwa Spika, unafiki uachwe kwenye mjadala wa mwaka huu tuweze
kuishauri na kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi kwa kuzingatia
maoni nitakayowasilisha.
“Mosi, spika aruhusu kabla ya mjadala huu kuendelea ziwekwe mezani
nakala ya ripoti zote za kamati za uchunguzi kwenye sekta ya nishati na
madini zilizoundwa na matokeo yake kutowasilishwa bungeni mpaka sasa.
“Pili, Wizara ya Nishati na Madini itakiwe kabla ya mjadala huu
kuwasilisha kabrasha la majibu ya michango ya wabunge juu ya makadirio
ya mwaka 2013/2014.
“Tatu, mara baada ya hoja hii kuamuliwa, naeleza kusudio la
kuwasilisha hoja binafsi ya kutaka kuundwe kamati teule ya kuchunguza
masuala tete na tata tuliyoyaeleza katika maoni haya ya Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni.
“Nne, Waziri Mkuu kwa mamlaka na madaraka yake kwa mujibu wa ibara ya
52 ya katiba ya nchi atakiwe katika mkutano huu wa Bunge kuelekeza
serikali iwasilishe taarifa bungeni juu ya maazimio ya Bunge kufuatia
uchunguzi uliofanyika kwa nyakati mbalimbali juu ya masuala yanayogusa
sekta za nishati na madini kama tulivyoyaeleza,” alisema Mnyika.
Wakichangia hoja hiyo, Kafulila, alisema kama Waziri Muhongo na
wenzake waliotuhumiwa katika kashfa hiyo ni wasafi, hawana sababu ya
kuogopa kuundiwa Kamati Teule kuwachunguza.
Mbunge huyo ambaye ndiye aliyeibua kashfa hiyo bungeni, alisema ana
ushahidi wa kutosha kuhusu kashfa hiyo na alipotakiwa na Spika Anne
Makinda kuwasilisha ushahidi alionao, aliinua begi zima lenye nyaraka
alizodai zinahusu namna wizi huo ulivyofanyika.
“Mheshimiwa Spika, hakuna dhambi mbaya duniani kama unafiki. Kama
kweli Bunge hili linataka kujua ukweli, tuunde Kamati Teule, watu
wametoa bilioni 200 kumpa Singasinga ambaye kule Kenya alikumbwa na
skandal ya Goldenberg iliyoiangusha Serikali ya Kenya.
“Ushahidi ninao, lakini kila nikitaka kuuleta spika anakatakata kona,” alisema Kafulila.
Alisisitiza kuwa kuunda Kamati Teule kuchunguza jambo hilo sio
kumsaka mchawi, hivyo Waziri Muhongo na wenzake hawana sababu ya kuwa na
wasiwasi.
Kafulila, ambaye aliwasilisha ushahidi wa tuhuma hiyo, alisema kwa
nchi makini, serikali pia ilitakiwa kufanya uchunguzi wa kifo cha Waziri
Mgimwa, kwani wakati amezidiwa na ugonjwa nchini Afrika Kusini, huku
nyuma fedha hizo zilichotwa kwenye akaunti hiyo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Simanjiro, Ole Sendeka, alipigilia msumari
kutaka Bunge liunde Kamati Teule kuchunguza ufisadi kwenye akaunti ya
Escrow.
Sendeka ambaye ni mbunge pekee wa CCM mwenye msimamo unaofanana na
kambi rasmi ya upinzani kwenye kashfa hiyo, alieleza jinsi fedha hizo
zilivyohamishwa Benki Kuu kwenda Benki ya Standard Chartered na jinsi
zilivyochotwa.
“Mheshimiwa Spika, kuna ushahidi wa namna vigogo walioshiriki kuchota
fedha hizo, walihamisha dola milioni 5, (sawa na sh bilioni 8), siku
nyingine watu wenye uhusiano na vigogo humu ndani walichota dola milioni
2, sawa na bilioni tatu), mara tano kwenye mifuko ya rambo na
kusafirisha kinyume cha sheria ya kutakatisha fedha,” alisema Sendeka.
Huku wabunge wa CCM wakimshangaa, Sendeka kwa kujiamini zaidi alisema
atawashangaa sana wabunge wa CCM watakaopinga kuundwa kwa tume hiyo ili
kujua ukweli.
Jioni, Sendeka alisema ana ushahidi wa wezi wa Tanzania ambao badala
ya kuwajibishwa wamekuwa wakipandishwa vyeo na wengine wamo ndani ya
Bunge akiwemo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na
Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi.
“Ninao ushahidi hapa unaonyesha fedha zilizochotwa Tanesco, wizara,
BoT na hata nikipigwa risasi nitaendelea kushikilia msimamo huo…
nitakupa ushahidi huo,” alisema.
Mnyika awasilisha ushahidi
Baada ya kutakiwa na spika kuwasilisha ushahidi mezani, Mnyika
aliwasilisha nyaraka mbalimbali kuthibitisha kashfa hiyo ya akaunti ya
Escrow.
Utoaji wa fedha za Escrow
Fedha za Escrow zilizotokana na malipo ya ‘capacity charges’,
zilikuwa katika makundi mawili; moja ni fedha za Kitanzania na za dola
za Marekani.
Kufikia Novemba 25, 2013, salio katika dola za Marekani, pamoja na
faida lilikuwa ni dola 22,198,544.60, wakati salio katika fedha za
Kitanzania lilikuwa ni sh 161,389,686,585.34, likijumuisha na faida
katika uwekezaji ambayo ilikuwa sh 5,297,550,682.04.
Ulipaji wa fedha za Escrow kwa IPTL
Kutokana na maelekezo ya IPTL, Novemba 28, 2013 fedha taslimu, dola
za Marekani 22,198,544.60 na shilingi 8,020,522,330.37 zililipwa katika
akaunti iliyotolewa na IPTL.
Desemba 5, 2013 BoT ilihamisha Hati Fungani (Treasury Bond) yenye
thamani ya sh 153,369,164,254.97 kwenda IPTL na kuhitimisha jukumu la
BoT la kuwa wakala wa Escrow.
Desemba 19, 2013, BoT iliiomba Wizara ya Fedha kufunga rasmi akaunti
ya Escrow kwa vile madhumuni ya kufunguliwa kwake yalifika mwisho.
Malipo ya Tanesco kwa IPTL
Wakati wa kufunga akaunti ya Escrow Desemba, 2013 Tanesco ilikuwa
ikidaiwa na IPTL dola za Marekani milioni 79.05 sawa na shilingi
bilioni 125.04 zilizotokana na ununuzi wa umeme (Capacity Charge) ambazo
hazijalipwa.