viongozi wa UKAWA |
Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa),Mwenyekiti wa CUF,Prof.Ibrahim Lipumba (Katikati),Mwenyekiti wa
Chadema,Freeman Mbowe(Kulia)na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi,James
Mbatia,wakionyesha alama ya vidole wakiashiria muungano wa serikali tatu
kwa wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika katika
viwanja vya Kibanda Maiti,mjini Zanzibar jana.Picha:Omar Fungo.
Vigogo wa Ukawa, wakiongozwa na Freeman Mbowe, Profesa Ibrahim Lipumba, James Mbatia, Tundu Lissu na Ismail Jussa Ladhu, na kuungwa mkono Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad na Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano, Hassan Nassoro Moyo, walisisitiza msimamo wa umoja huo wa kutaka kuwapo mabadiliko ya kuwapo mfumo wa Muungano wa serikali tatu.
Msimamo huo ulisisitizwa jana katika mkutano wa hadhara, ambao ni wa kwanza wa umoja huo kufanyika tangu wafuasi wake waamue kujitoa katika Bunge hilo, uliohudhuriwa na maelfu ya watu mjini Unguja na vitongoji vyake, katika uwanja wa Demokrasia Kibandamaiti.
HASSAN NASSORO MOYO
Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano, Hassan Nassoro Moyo, alisema serikali tatu ndiyo msimamo wa Wazanzibari na kwamba, hawawezi kubadilika.
Alisema walichagua kuungana na Watanganyika kwa sababu ya maisha ya Wazanzibari.
MAALIM SEIF
Katibu Mkuu wa Cham cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), alisema serikali tatu hazina mjadala.
Hivyo, akasema kwa kuwa wenzao (CCM) wamekuwa waking’ang’ania mfumo wa Muungano wa serikali mbili, anaukubali, lakini kwa sharti kwamba, Zanzibar inakuwa huru.
Maalim Seif alisema kama gharama ndizo zinazoogopwa, basi kila mtu awe na serikali yake.
Aliwashukuru viongozi wa Ukawa kwa kuonyesha uongozi katia Bunge hilo na kusema wanaojiita wengi wameonekana wengi hivyo na wanaonekana wachache wameonekana wachache makini.
Alisema Wazanzibari wanawaunga mkono mia kwa mia na kwa uamuzi waliyoyachukua ya kuondoka bungeni, kwa kuwa ni uamuzi wa kijasiri na hekima.
Maalim Seif alisema anajua zitafanywa juhudi zote kuvunja umoja wao, kwa kutumia fedha na vitisho, lakini akawataka waendelee kuulinda umoja wao kama mboni ya jicho.
Aliwataka kuulinda umoja wao na kuwa makini kwa kuwa hao hawana hoja kwa kuwa mfumo wanaoutetea ni wa dhuluma na wao wanatetea mfumo wa haki na kwamba, watashinda na hilo hana wasiwasi nalo hata kidogo.
Alisema anashangazwa kutajwa katika Bunge hilo wakati yeye siyo mbunge.
“Msikubali na tusikubali kugawiwa,” alisema Maalim Seif.
Alisema msimamo wake ni ule wa Ukawa na kwamba, yeye hana historia ya kuwasaliti wananchi na hayuko tayari kwa hilo.
Maalim Seif alisema Muungano uliopo ni wa nchi mbili na kwamba, kauli ya baadhi ya viongozi wa serikali kwamba, hawawezi kuiacha Zanzibar na kuhoji “Je, Zanzibar ni koloni lenu?”
Alitoa mfano wa Algeria, ambako wakoloni Wafaransa waligoma kuiachia huru nchi hiyo, lakini mwisho wake waliondoka na kuiacha.
Alisema wakati wa kutishana umekwisha na kwamba vitisho vyao haviwezi kuwarudisha nyuma Wazanzbari.
“Serikali mbili mnazozitaka nyinyi, tunasema no,”alisema.
Kuhusu vitisho vya kumdhibiti yeye (Maalim Seif), alisema kamwe hilo hawaliwezi.
Alisema anayo taarifa kwamba, askari wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM) na Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ) wamekuja katika eneo la mkutano wakiwa wamevalia kiraia ili wawasumbue wananchi barabarani baada ya mkutano.
Alisema yeye kama Makamu wa Kwanza wa Rais, anaamuru askari hao waondolewe mara moja eneo hilo, vinginevyo watamjua Maalim Seif kuwa ni nani?
JAMES MBATIA
James Mbatia ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi na Mbunge wa Kuteuliwa na Rais aliwaonya wawakilishi wa Ukawa Zanzibar juu ya kitendo cha kuiuza Zanzibar ili kujenga uhusiano mwema kati yao na wenzao wa Tanganyika.
“Tusikubali katu katu hatua tuliyofikia kurudi nyuma, Mwenyezi Mungu atatoa baraka zote na kugombana naye, ” alisema Mbatia.
FREEMAN MBOWE
Freeman Mbowe, ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema na Mbunge wa Hai, alisema kauli kwamba, Ukawa wakirudi kwa wananchi watachekwa ni dalili kwamba, utawala umekosa busara.
Alisema leo wataendelea na mikutano kisiwani Pemba na baada ya hapo watakwenda jijini Dar es Salaam kuhakikisha haki ya wananchi inapatikana.
Mbowe alisema Zanzibar ndiyo itakayoonyesha njia ya kufanikisha harakati za kufikia lengo la kuwapo kwa mfumo wa serikali tatu.
Alisema wako tayari kuendelea kutukanwa, lakini watatembea nchi nzima kuhakikisha wanadai haki za Watanzania, ikiwamo serikali tatu.
KUVUNJA BARAZA LAMAWAZIRI
Alisema ushirika uliopo baina vyama vyao hivi sasa, hautaishia tu katika kudai katiba ya wananchi, bali utaendelea hadi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia na katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015.
Mbowe alisema kwa kuzingatia hilo, wiki ijayo atavunja baraza la mawaziri kivuli linaloundwa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na kuliunda upya ili kuhakikisha Ukawa inasambaa siyo katika Bunge Maalumu la Katiba tu, bali unaendelea pia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na katika Uchaguzi Mkuu mwakani.
“Nina imani mwaka 2015 tunaendelea kuzungumza, tutakwenda kwenye uchaguzi tukiwa kitu kimoja,” alisema Mbowe.
PROFESA LIPUMBA
Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye ni Mwenyekiti wa CUF na Mjumbe wa Bunge hilo, alisema kinachopiganiwa na Ukawa siyo katiba ya chama chochote cha siasa, bali ya wananchi, hivyo akasema wataendelea kuidai na kudai pia kutekelezwa matakwa yao.
Alisema Ukawa inaunga mkono kauli ya Mbowe na viongozi wengine wa umoja huo kuhusu umuhimu wa wafuasi wa Ukawa kuungana siyo katika kudai tu katiba ya wananchi, bali pia katika kupata serikali imara mwakani.
ISMAIL JUSSA LADHU
Mjumbe wa Bunge hilo, ambaye ni Mwakilishi wa Mjimkongwe (CUF), Ismail Jussa Ladhu, alisema kwa miaka mingi Wazanzibari wamekuwa wakiwashuhudia wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar wakiwa kitu kimoja, lakini walipofika Dodoma wakashuhudiwa wakiufyatana kuhoji sababu za ukali wao kuishia katika baraza hilo.
Alisema alichogundua ni kuwa kinachowasumbua watu hao ni matumbo yao badala ya maslahi ya Wazanzibari.
Aliwataka Wazanzibari kuhakikisha wanalipiza kisasi dhidi ya usaliti unaodaiwa kufanywa na watu hao aliowaita kuwa ni wasaliti na wanafiki.
Alisema inasikitisha kuona leo haki za Wazanzibari zinatetewa na wananchi wa Tanzania Bara, kama Lissu, Mnyika na Mbatia, badala ya Wazanzibari wenyewe.
MOSENA NYAMBABE
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, ambaye ni mmoja wa viongozi wa Ukawa nje ya Bunge, Mosena Nyambabe, alisema fursa ya kutunga katiba mpya ni fursa ambayo tangu kupatikana kwa uhuru Watanzania hawajawahi kushirikishwa katika hilo.
Hivyo, alisema daima hawako tayari kukubali CCM kuwarudisha kwenye katiba ya zamani baada ya kuikarabatina kuiwekea viraka, bali wanachokitaka ni katiba mpya.
DK. WILLIBROD SLAA
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, alisema Watanzania wanasubiri matokeo ya mkutano wa leo baada ya Ukawa Nje ya Bunge kuzunguka mikoa kadhaa hadi vijijini, ambako kote alisema hawana chaguo linguine zaidi ya kutaka serikali tatu.
Alisema madai kwamba, waliozaliwa baada ya mwaka 1964 hawaijui Zanzibar ni ya upotoshaji mkubwa.
Dk. Slaa pia alisema pia madai kwamba, zikipitishwa serikali tatu jeshi litachukua nchi, halina msingi kwa kuwa kuna fedha, ambazo ni mishahara na posho za wanajeshi zilikatwa, lakini hawakupindua serikali.
DK. MAKAIDI
Mwenyekiti wa NLD, ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge hilo, Dk. Emmanuel Makaidi, alisema katika serikali tatu kuna imani tatu; ya wananchi, ya Mungu na uzalendo, lakini hakuna imani yoyote.
MCHUNGAJI MTIKILA
Mchungaji Christopher Mtikila, ambaye pia Mjumbe wa Bunge hilo, alisema Zanzibar walitangulia kupata akili tofauti na wenzao Watanganyika.
TUNDU LISSU
Mjumbe Tundu Lissu alisema kwa nusu karne Zanzibar haijawa huru, badala yake imekuwa koloni la Tanganyika.
Alisema hali hiyo inatokana na masuala yote ya Zanzibar ya mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa, ulinzi, uchumi, fedha, sarafu, mabenki na benki kuu, kwa miaka yote hiyo kuendelea kuamuliwa jijini Dar es Salaam.
Alisema Zanzibar haiku huru, basi na Tanganyika nayo pia haiwezi kuwa huru kwa kuwa hakuna mahali popote katika kumbukumbu za serikali kuna jina Tanganyika na kusema kuwa Watanganyika wameamua kukana uwapo wa Tanganyika ili waendelee kuikalia Zanzibar.
“Bila Zanzibar huru Tanganyikahaiwezi kuwa huru,” alisema Lissu.
Alisema makubaliano ya Muungano hayakuua nchi hizo mbili, hivyo akasema madai kwamba, kuna nchi moja ni uwongo.
Lissu alisema baada ya nusu karne ya kutawaliwa Wazanzibari wameamka, wanataka Zanzibar huru yenye mamlaka kamili, itawakomboa pia Watanganyika kwa kuwa wote watakuwa wote huru na hivyo, watakuwa wanafanya mambo kwa misingi ya haki sawa, tofauti na sasa.
“Umefika wakati wa kupata mamlaka kamili ya Zanzibar ili kuwatoa Watanganyika mafichoni,” alisema Lissu.
Aliwaomba Wazanzibari wawaongoze tena Watanganyika kile walichowaongoza miaka 30 iliyopita wakati wa harakati za Mapinduzi yaliyoung’oa madarakani utawala wa kisultani visiwani humo.
Alisema hiyo ni kwa kila Mzanzibari kuhakikisha anamkaba rafiki, jirani na mbunge wake, ambaye ni mjumbe wa Bunge hilo kuhakikisha Zanzibar huru inapatikana.
PROF. ABDUL SHARIF
Mjumbe wa Bunge hilo, Profesa Abdul Sharif, aliwataka wananchi kuwa pamoja akisema ndiyo njia pekee ya kufikia mafanikio ya kile wanachokitafuta katika mchakato wa kupata katiba mpya iliyobora.
No comments:
Post a Comment