Dar es Salaam. ‘Nenda, rudi’ za kipa wa Yanga, Ally Mustapha
‘Barthez’ zinakaribia kutimia baada ya kipa huyo kuanza mazungumzo na
Simba ili arejee tena Mtaa wa Msimbazi kuichezea klabu hiyo kwa mkataba
wa miaka miwili.
Kipa huyo alishajiunga na Yanga mara mbili
akitokea Simba na endapo atasaini mkataba atakuwa akirejea kwa mara ya
pili akitokea Jangwani.
Katibu mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema
kocha wa timu hiyo, Zdravko Logarusic ndiye aliyependekeza Barthez
asajiliwe ili kuongeza nguvu katika kikosi chao msimu ujao baada ya
kuvutiwa na kiwango chake.
“Kocha ametaka msimu ujao awe na kikosi
kisichozidi wachezaji 25, na katika mapendekezo yake alisema lazima
Barthez asajiliwe, na tayari tumeshaanza mazungumzo na Barthez, huenda
tukampa mkataba wa miaka miwili,” alisema Kamwaga.
Barthez ambaye amekuwa na wakati mgumu wa kupata
nafasi kwenye kikosi cha Yanga hivi sasa, imeelezwa kuwa ameshaafikiana
na Yanga kuwa anamalizia mkataba wake kisha atatua Simba, ambao
amezungumza nao na tayari wamekubaliana asaini mkataba wa miaka mwili.
Mlinda mlango huyo ambaye pia alishawahi kuichezea
Simba na kusoteshwa benchi kwa miaka mitatu na Juma Kaseja kabla ya
kutimkia Yanga na kupanda chati kuwa kipa tegemeo ndani ya klabu hiyo,
alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kufungwa mabao matatu katika
mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba iliyomalizika kwa sare ya mabao
3-3.
No comments:
Post a Comment