Thursday, 1 May 2014

Kura zaanza kuhesabiwa Irak

Zoezi la kuhesabu kura linaendela nchini Irak baada ya uchaguzi wa jana ambao ulikabiliwa na mashambulizi. Uchaguzi huo umesifiwa na Umoja wa Mataifa na Marekani, ukitajwa kuwa karipio wa wanaotaka vita vya kijihadi.
Zoezi la kuhesabu kura litaendelea kwa majuma mawili Zoezi la kuhesabu kura litaendelea kwa majuma mawili
Takwimu za awali zilizotolewa na tume ya uchaguzi ya Irak zimeonyesha kuwa asilimia 60 ya watu milioni 20 wenye haki ya kupiga kura nchini Irak, ndio walioitikia uchaguzi huo, ikiwa na upungufu wa asilimia 2 ikilinganishwa na waliojitokeza kupiga kura zao katika uchaguzi wa mwaka 2010.
Matokeo ya kwanza yatatolewa katika kipindi cha majuma mawili, na waziri mkuu Nuri al-Maliki anatarajiwa kuibuka mshindi licha upinzani mkubwa unaomkabili, ikiwa ni pamoja na kutoka ndani ya jamii ya washia anakotoka. Uchaguzi wa jana ni wa kwanza nchini Irak tangu kuondoka kwa wanajeshi wa Marekani nchini humo, na umefanyika huku taifa likikumbwa na mlolongo wa machafuko. Mashambulizi ya siku ya uchaguzi yaliwauwa watu 14, wakiwemo maafisa wawili wa uchaguzi.
Karipio kwa wachochezi wa ghasia
Kipindi cha kampeni kiligubikwa na mlolongo wa mashambulizi Kipindi cha kampeni kiligubikwa na mlolongo wa mashambulizi
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry ameusifu uchaguzi huo, na kusema umetuma ujumbe wenye nguvu kwa makundi yenye misimamo mikali ambayo yanaazimia kuupotosha mchakato wa demokrasia katika nchi hiyo. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitolea rai Irak kuunda serikali itayowakilisha matakwa ya watu wa Irak, haraka iwezekanavyo.
Katika tangazo lake Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesema hakuna kiwango cha ugaidi na matumizi ya nguvu, ambacho kinaweza kuurudisha nyuma mpango wa kuikarabati demokrasia ndani ya Irak, ambayo inajengwa kwa msingi wa sheria na kuheshimu haki za binadamu.
Akizungumza baada ya kupiga kura yake jana, waziri mkuu wa Irak Nuri al-Maliki aliwaambia waandishi wa habari mjini Baghdad kwamba anao uhakika wa kupata ushindi. ''Hatuna mashaka yoyote kuhusu ushindi, ila tunasubiri tu kujua utakuwa ushindi wa kiasi gani'' Alisema kiongozi huyo.
Gharama ya demokrasia
Waziri Mkuu wa Irak Nuri al-Maliki anatarajiwa kupata ushindi Waziri Mkuu wa Irak Nuri al-Maliki anatarajiwa kupata ushindi
Wachambuzi wa masuala ya Irak walikuwa wametabiri kwamba raia wengi wangeamua kubaki majumbani mwao kuliko kwenda kwenye vitua vya kura ambavyo vilikabiliwa na hatari ya kushambuliwa. Hata hivyo wengi walijitokeza wakisema wamechoshwa na viongozi wao.
Mkongwe mmoja mwenye umri wa miaka 91 Jowad Kamal al-Din alisema anayo matumaini kwamba Irak inao mustakabali wenye amani, ambamo tatizo la ukosefu wa ajira litashughulikiwa ipasavyo, na sekta za kilimo na viwanda kurejea katika hali yake ya awali na hivyo kupunguza utegemezi kwa sekta ya mafuta.
Mkongwe huyo pia alielezea matumaini kuwa viongozi wa sasa hasa wabunge ambao aliwataja kuwa wezi, wataondolewa katika uchaguzi huu.
Wapinzani wa waziri Mkuu Nuri al-Maliki wanasema kiongozi huyo amejilimbikizia madaraka, na kuwatenga watu wa madhehebu ya sunni ambao ni wachache nchini Irak. Wanasema vile vile kuwa huduma kwa jamii hazikuboreka chini ya utawala wake wa miaka minane iliyopita.
Kwa upande wake al-Maliki ameulaumu mgogoro wa Syria kwa ghasia zinazoendela nchini mwake, na kuzinyoshea kidole nchi za Qatar na Saudi Arabia zenye wasuni wengi kuunga mkono waasi nchini Irak.

No comments: