Thursday, 8 May 2014

Gari chakavu lazua tafrani Bungeni Tanzania

Maofisa usalama wa Bunge wakishirikiana na Jeshi la Polisi jana saa 3:40 asubuhi walilizingira gari moja la Serikali lililokuwa limeegeshwa ndani ya eneo la Bunge.
Gari hilo ambalo linaonekana kuwa chakavu kiasi, aina ya Toyota Prado lilizingirwa na maofisa hao ambao walilizungushia kamba maalumu za njano zenye maandishi ‘Crime Scene’ yakimaanisha ni eneo la tukio la jinai.
Kamba hizo zimekuwa zikitumiwa na Jeshi la Polisi kuzuia watu wasiohusika na masuala ya kiusalama kusogelea eneo hilo ili kutoa fursa kwa wataalamu kufanya uchunguzi ikiwamo kuchukua sampuli.
Mwandishi wetu aliwashuhudia maofisa hao wakitumia mbwa weusi kulikagua gari hilo.
Hata hivyo, haijafahamika ilikuwaje gari hilo kuwa eneo hilo ambalo hutumika kwa maegesho ya magari binafsi ya wabunge na viongozi na huduma za kibiashara.Kwa utaratibu, magari yote yanayoingia ndani ya viwanja vya Bunge hufanyiwa ukaguzi maalumu na mitambo iliyopo katika mageti.
Wakati wa ukaguzi huo, maofisa hao walianza kutoa amri kwa watu waliokuwa karibu na eneo hilo, wakiwamo wanahabari kuondoka.
“Tunawaomba muondoke eneo hili kwa sababu kuna shughuli maalumu tunaifanya,” alisema ofisa mmoja.
Habari ambazo hazijathibitishwa zilieleza wakati wa ukaguzi huo, maofisa hao waliokota kitu kisichojukana na kukichukua kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma ambaye pia alikuwa katika eneo la tukio, David Misime alisema baadaye kuwa hajui chochote kuhusu jambo hilo.

No comments: