Ajali
Tumefikia mahali sasa kwamba tumekuwa taifa la
maombolezo kutokana na ajali za barabarani zinazotokea kila kukicha na
kupukutisha maisha ya watu, huku zikiacha maelfu ya majeruhi wakiwa na
vilema vya maisha na kulazimika kuanza maisha mapya ya utegemezi.
Hatuhitaji kuorodhesha hapa majina ya watu waliopoteza maisha au kupata
vilema vya maisha kutokana na ajali za barabarani miezi minne tangu
mwaka huu uanze. Kuorodhesha majina hayo siyo tu tutakuwa tunatonesha
vidonda na kuwanyong’onyeza jamaa zao, bali pia orodha hiyo ni ndefu mno
kiasi cha kutoweza kuenea katika nafasi finyu ya safu hii.
Sababu nyingine ya kutoorodhesha majina ya
waathirika hao wa ajali ni ukweli kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba
tumepoteza hesabu yao. Ajali za barabarani zimekuwa nyingi mno kila kona
ya nchi kiasi kwamba hata Serikali inaonekana kutokuwa na uhakika wa
idadi kamili ya waathirika wa ajali hizo. Kinachojitokeza sasa ni hali
ya Serikali kukata tamaa pengine baada ya kushindwa kwa muda mrefu
kupata mkakati na mbinu za kuzikomesha au kuzipunguza . Ndiyo maana kwa
muda mrefu sasa imekuwa kimya kama vile haijaguswa na ajali hizo, ikiwa
ni pamoja na iliyotokea juzi mkoani Singida.
Tunadhani kuna haja sasa kwa Serikali kutafakari
kwa kina sababu za kuongezeka kwa ajali za barabarani kwa kiwango hicho.
Lazima ikubali kwamba sheria zilizopo na mikakati na mbinu zinazotumiwa
kukomesha ajali hizo zimepitwa na wakati au zinakosa usimamizi na
utekelezaji thabiti na makini. Kwa kuwa hivi sasa hali ya barabara zetu
nyingi ni ya kuridhisha, tungetarajia ajali za barabarani zipungue
badala ya kuongezeka.
Serikali pia ijitathmini wapi imekosea katika
kusimamia sheria husika. Mikakati yake imekuwa ya zimamoto. Mpango wa
kutumia vidhibiti mwendo (speed governor) vya magari ulikufa katika
mazingira ya kutia shaka. Hivi sasa kuna tatizo la usalama. Magari
yanatekwa na majambazi, hivyo madereva wanaendesha kwa kasi wakihofia
kutekwa, hasa nyakati za usiku. Serikali isikate tamaa wala kuinua
mikono. Iongeze idadi ya askari wa usalama barabarani, iwape mafunzo na
vifaa na ihakikishe ni waadilifu.
Tunapendekeza kamera za usalama zifungwe
barabarani, utoaji holela wa leseni za madereva udhibitiwe na wamiliki
wa magari wabanwe ili wafunge mitambo ya kufuatilia mwenendo wa magari
yao yanapokuwa safarini. Wamiliki hao pia wabanwe wakate bima
zitakazowawezesha waathirika wa ajali kulipwa fidia. Ni matumaini yetu
kwamba Serikali ikisimamia sheria kikamilifu na kutoa elimu ya uraia ili
wananchi wajione ni sehemu ya suluhisho, ajali za barabarani zitabaki
kuwa historia.
No comments:
Post a Comment