Thursday, 1 May 2014

Waziri wa Fedha: Bajeti ya mwaka 2014/2015 ni Sh19.6 trilioni

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiteta jambo na  Waziri wa Fedha, Saada Mkuya kwenye mkutano wa wabunge ambapo waziri wa fedha aliwasilisha mapendekezo na mwelekeo wa bajeti ya serikali  kwa mwaka fedha 2014/15, Dar es Salaam jana

Wakati  bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2014/15 ikitarajiwa kuongezeka kutoka Sh. trilioni 18.2 za mwaka huu hadi trilioni 19.6, serikali imeelezea wasiwasi wa kukwama kwa baadhi ya shughuli za  mwaka huu wa fedha kutokana na uhaba wa fedha.

Hali hiyo ilielezwa jana na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, alipokuwa akiwasilisha mwelekeo wa bajeti ya mwaka wa fedha unaokuja na utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu wa fedha unaotarajiwa kumaliza mwisho wa mwezi ujao.

Akiwasilisha mwelekeo huo jana kwa wabunge jijini Dar es Salaam, Mkuya alisema katika mwaka ujao wa  fedha serikali itatumia Sh. trilioni 19.6 ikiwa ni ongezeko la Sh. trilioni 1.4 ikilinganishwa na mwaka huu wa fedha.

Sababu zilisababisha upungufu wa mapato kwenye bajeti ya serikali ni pamoja na kuondoa tozo la kodi ya kadi za simu (SIMcard) iliyopendekezwa mwaka jana kwenye bunge la bajeti.

Waziri Mkuya alisema utekelezaji wa bajeti kwa mwaka jana kuanzia Julai 2013 hadi Machi mwaka huu umekumbwa na changamoto nyingi, ikiwamo kushuka kwa ukusanyaji wa mapato na baadhi ya wahisani kutochangia bajeti hiyo kama walivyoahidi.

Alieleza kuwa hali hiyo inaleta wasiwasi wa kumaliza mwaka kukiwa na upungufu katika mapato ya serikali.

“Katika kipindi hicho mapato yote ya serikali yalikuwa Sh. trilioni 11 sawa na asilimia 93 ya makadirio ya mwaka 2013/14,” alisema na kuongeza kuwa  kuna upungufu wa asilimia saba kwenye bajeti hiyo na kwamba endapo mwenendo huo utaendelea bila kudhibitiwa, kuna uwezekano wa kumaliza mwaka wa fedha 2013/14 na nakisi ya bajeti.

NIPASHE iliomba ufafanuzi wa maelezo hayo kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk.  Servacius Likwelile, aliyetafsiri kuwa kuna ukosefu wa  fedha unaoweza kukwamisha  utekelezaji wa miradi ya maendeleo na shughuli za kawaida za uendeshaji wa serikali ambazo ni  pamoja na kutoa huduma na kulipa mishahara.  

Hata hivyo, alisema hatua zinachukuliwa ili kuzuia hali hiyo isitokee.

HATUA ZA KUZUIA KUKWAMA
Waziri wa Fedha alizitaja baadhi ya hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa kuwa ni kukusanya marejesho ya kodi kutoka kampuni za Shoprite na Vodacom, kufuatilia Dola milioni 85  kutoka kwa wahisani wanaochangia bajeti ya serikali (GBS), kufuatilia Dola milioni 100 zilizoahidiwa na wahisani kwa ajili ya sekta ya nishati na kukusanya mapato yasiyo ya kodi kutoka wakala na taasisi nyingine za serikali.

UKWAMISHAJI MAPATO

Waziri Mkuya aliyataja baadhi ya mambo yaliyokwamisha ukusanyaji mapato kuwa ni makusanyo hafifu ya kodi kutoka kwenye makampuni (corporate tax) hasa kampuni za madini yaliyosababishwa na kushuka kwa bei ya dhahabu kwenye soko la dunia. Dhahabu ndiyo inayoongoza kuipatia Tanzania fedha za kigeni.

Kadhalika, alisema kampuni za simu za mikononi hazikukusanya tozo ya kadi za simu iliyotarajiwa kuliingizia taifa Sh. bilioni 178 katika mwaka huu wa fedha.

“Licha ya makadirio ya kiasi hicho, hadi kufikia Desemba mwaka jana hakukuwa na kiasi chochote cha kodi ya SIM card kilichokuwa kimekusanywa, hivyo kuongeza pengo la mapato,” alisema Waziri Mkuya.

Alieleza kuwa baada ya kodi hiyo kupingwa na wananchi na wadau mbalimbali, Bunge lilibadilisha sheria ya kodi ya tozo ya simu card na kuifanya kuwa nyongeza kwenye ushuru wa bidhaa za  kodi ya simu.

Alifafanua kuwa kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu Sh. bilioni 14.03 zilikusanywa kama fidia kutoka kwenye makampuni ya simu  kutoka Tanzania Bara na Sh. bilioni moja kutoka Zanzibar.

Hata hivyo, Waziri wa Fedha alisema jitihada nyingine zinazochukuliwa ni kupunguza na kudhibiti misamaha ya kodi isiyo na tija kwa taifa

AHADI ZA GBS

Akizungumzia GBS na upungufu wa mapato, alisema kuanzia Julai 2013 hadi Machi mwaka huu, wahisani wanaochangia bajeti ya serikali (GBS) na washirika wengine wa maendeleo walikuwa wamechangia Sh. trilioni 1.1  ambayo ni nusu (asilimia 50) ya kiasi walichoahidi cha Sh. trilioni 2.3.

Mkuya alisema kuanzia Julai 2013 hadi Machi mwaka huu, serikali ilikopa Sh. bilioni 776.5 kutoka makadirio ya Sh. bilioni 820 zilizopangwa kukopwa kwa ajili ya kulipia hati fungani na amana za serikali zilizoiva.

MISINGI YA BAJETI 2014/15
Akielezea misingi ya bajeti kwa mwaka ujao, Mkuya alisema ni pamoja na kuimarisha amani, usalama, utulivu na utengamano.

Pia itaelekezwa kwenye mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya, kufanikisha  uchaguzi mkuu wa mwakani wa Rais na wabunge na serikali za mitaa.

Alisema sera za fedha zitaendelea kuimarishwa ili ziendane na sera za bajeti zitakazosaidia kupunguza mfumuko wa bei na tofauti ya riba za amana na za mikopo.

SERA ZA MAPATO 2014/15

Waziri Mkuya alisema zimelenga  kuongeza mapato, kuimarisha taratibu za ukusanyaji wake, kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi hadi ifikie asilimia moja ya pato la taifa.

“Nyingine ni kuendelea na utekelezaji wa mapendekezo ya mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN), pamoja na kukamilisha utungwaji wa sheria ya kodi, kufanya mapitio  ya kodi ya ongezeko la thamani (Vat) ili kuchangia kuongeza pato la taifa.

Nyingine ni kuongeza kasi ya kupunguza au kuondoa kabisa mogogoro ya ardhi ili serikali ikusanye mapato kutoka kodi za viwanja na majengo.

Itakuwa pia kwenye vipaumbele vya taifa ambavyo ni kilimo, elimu, maji, utafutaji wa rasilimali fedha, nishati na uchukuzi na uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara.

WAZIRI MKUU

Akitoa hali ya utekelezaji wa bajeti mwaka jana, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema bajeti ya 2013/14, ilikuwa ngumu na kuelezea kuwa matarajio waliyoyaweka serikalini hayajafikiwa.

Alisema bajeti hiyo ilikuwa na changamoto nyingi kwani serikali ilianza mwaka wa fedha wa 2013/14 kwa deni.

“Japokuwa bajeti ya mwaka huo na mwaka ujao inatofautiana kwa Sh.  trilioni 1 ni matarajio yetu kuanza mwaka ujao wa fedha tukiwa tumemaliza madeni ya mwaka jana,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema malengo ya sasa ni kuachana na utegemezi na kwamba jitihada zimefanywa na sasa fedha za ndani zimefikia asilimia 63 ya bajeti na serikali inaendelea kupunguza utegemezi.

Alisema lengo kubwa ni kupata umeme kwa kukamilisha ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ili viwanda vizalishe kwa uhakika na vingine vianzishwe hatua itakayoliingizia taifa mapato.

WASSIRA

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira, akiwasilisha rasimu ya mpango wa maendeleo wa taifa kwa mwaka 2014/15 na alisema hadi kufikia Desemba 2013 deni la taifa lilifikia Sh. trilioni 27.

Alisema kati ya deni hilo, deni la nje lilikuwa Sh. trilioni 20.23 ikiwa ni asilimia 74.8 ya deni la taifa wakati  kati ya deni la nje deni la serikali ni Sh. trilioni 16.7 na deni la sekta binafsi ni Sh. trilioni 3.5.

Aidha, alisema deni la ndani lilifikia Sh. trilioni 6.81 sawa na asilimia 25.2 ya deni la taifa, na kufafanua kuwa ongezeko la deni la taifa lilitokana na mikopo mipya ya kibiashara na ya masharti nafuu iliyopokelewa na serikali pamoja na malimbikizo ya riba.

Bunge la bajeti linatarajiwa kuanza Jumanne ijayo na bajeti ya serikali itasomwa Juni 12, mwaka huu.

No comments: