SERIKALI
imebanwa itoe ufafanuzi wa utata uliojitokeza katika Wizara ya
Maliasili na Utalii, baada ya Katibu Mkuu, Maimuna Tarishi kutengua
uamuzi wa waziri wake, Lazaro Nyalandu na kuwarejesha kazini vigogo wa
Idara ya Wanyamapori waliokuwa wameng’olewa.
Waziri Nyalandu aliwang’oa Mkurugenzi wa Wanyamapori, Profesa
Alexander Sorongwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Matumizi Endelevu ya
Wanyamapori, Jafari Kidegesho, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa azimio
la Bunge la Desemba 22, mwaka jana.
Azimio hilo lilifikiwa baada ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili
na Mazingira chini ya Mwenyekiti wake, James Lembeli, kuwasilisha ripoti
ya utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili na kuonyesha kuwa
watendaji wa Maliasili, wakiwemo vigogo hao, walizembea hadi wananchi
wakatendewa unyama na wengine kupoteza maisha na mali zao.
Bunge liliitaka serikali iwawajibishe watendaji wote waliozembea,
akiwemo Prof. Sorongwa, ambaye alielezwa kuwa alitoa taarifa zisizo
sahihi juu ya kuteswa kwa baadhi ya raia hao wema.
Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida, Katibu Mkuu, Tarishi,
hivi karibuni kwa maelekezo ya Ikulu, alitengua uamuzi wa waziri wake na
kuwarejesha vigogo hao kazini.
Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM), aliibana serikali itoe
kauli juu ya mgogoro unaoendelea katika wizara hiyo akidai umeibua utata
mkubwa.
Akichangia hotoba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa
fedha 2014/2015 jana, Shellukindo alisema kuwa Waziri Nyalandu alimtimua
Mkurugenzi wa Wanyamapori, lakini hivi karibuni mamlaka nyingine
imemrejesha kazini katika mazingira yanayoibua maswali.
Shellukindo alisema kung’olewa kwa mkurugenzi huyo kulitokana na
mapendekezo ya Azimio la Bunge lililobaini madudu katika Operesheni
Tokomeza Ujangili.
“Mheshimiwa Spika, mkurugenzi aling’olewa kutokana na mapendekezo ya
Bunge. Leo amerudishwa, basi hata Waziri wa Maliasili na Utalii
aliyeng’olewa kwa sababu hiyo hiyo, naye arejeshwe,” alisema.
Kwa mujibu wa Shellukindo, wizara hiyo ni muhimili mkubwa wa pato la
taifa, hivyo alimtaka Waziri Mkuu kutoa maelezo juu ya nini kinaendelea
katika wizara hiyo.
Katika hatua nyingine, wabunge mbalimbali bila kujali itikadi zao,
jana waliungana kutetea operesheni kamata vijana waendesha bodaboda
ambao wamekuwa wakifanya kazi zao katika mazingira magumu katika miji
mikubwa nchini.
Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam ndio waliokuwa wa kwanza kuwasha moto kuwapigania bodaboda.
Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu (CCM), alisema operesheni hiyo imekuwa
ikiendeshwa kibabe na uonevu kwani hata walemavu wanakamatwa kwa
kisingizio cha kusafisha jiji.
Zungu alisema kibaya zaidi vijana wanaokamatwa na bodaboda wamekuwa wakipigwa faini ya hadi sh 100,000 kwa makosa ya uonevu.
Abbas Mtevu, Mbunge wa Temeke (CCM), alisisitiza kuwa hakuna mbunge
anayetaka uchafu, lakini jijini Dar es Salaam, wabunge hawakuwa na
taarifa juu ya operesheni hiyo.
Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM), alisema kuwa Bunge lilifuta
ushuru wa bodaboda ili waweze kupata faida, lakini faini wanazotozwa
sasa zimesababisha biashara zao kuwa ngumu.
Godbless Lema, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), alisema kuwa
serikali ikiamua kuwaondoa wamachinga na bodaboda nchi itawaka moto.
Alisema kuwa kundi hilo likiondolewa mchana, usiku wataamua kufanya kazi nyingine na hakuna atakayepona.
Aliilaumu serikali kuwa tatizo la wamachinga ni kutokana na mipango
dhahifu ya serikali ambayo imekuwa ikitegemea misaada kuendesha bajeti
yake.
No comments:
Post a Comment