Saturday, 10 May 2014

Wakulima wapewe fidia asema Silinde

MBUNGE wa Mbozi Magharibi, David Silinde (Chadema), ameitaka serikali kuwafidia wakulima wa Mbozi ambao mazao yao yaliungua kutokana na kutumia mbolea feki.
Akiuliza swali la nyongeza bungeni jana, Silinde alisema wakulima hao walinunua mbolea hizo katika kampuni mbalimbali za usambazaji wa mbolea.
“Serikali ina mpango gani wa kuwalipa fidia wakulima hao ambao mazao yao yote yaliungua kutokana na matumizi ya mbolea feki?” alihoji Silinde.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi, alisema ni kweli wananchi wa Mbozi na maeneo mengine nchini mazao yao yaliathiriwa kutokana na matumizi ya mbolea isiyokidhi viwango.
Aliwahimiza wakulima wanaponunua mbolea kudai stakabadhi, ili iwe rahisi kufanya ufuatiliaji.
“Iwapo ikithibitika kwamba mbolea aliyoitumia mkulima imesababisha mazao hayo kuungua, serikali itakuwa tayari kufidia,” alisema.
Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kiembe Samaki, Waride Bakari Jabu (CCM), Zambi alisema utaratibu wa uteketezaji wa mbolea hizo zisizokidhi viwango unahitaji kufanyika kwa umakini wa hali ya juu kutokana na mbolea hizo kuwa na kemikali.
“Mamlaka ya Mbolea kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mkemia Mkuu wa Serikali inakamilisha mwongozo na taratibu za kitaalamu zitakazotumika kusimamia uteketezaji wa mbolea zisizo na viwango nchini,” alisema Zambi.
Katika swali lake, Jabu alitaka kujua utaratibu unaotumika kuteketeza mbolea feki ili kulinda afya za wananchi na uhifadhi wa mazingira.

No comments: