Saturday, 10 May 2014

Mashine 12 kutua Simba

KAMATI ya Usajili ya Simba imeanza mchakato wa kusajili wachezaji 12 wa kuziba nafasi zitakazoachwa wazi na wachezaji waliopendekezwa kutemwa na ripoti ya benchi la ufundi lililo chini ya Mcroatia, Zdravko Logarusic, huku jina la kipa Ally Mustapha 'Barthez' likitajwa.
Logarusic katika ripoti yake aliyoiwasilisha mwishoni mwa mwezi uliopita kabla ya kwenda mapumzikoni kwao, alipendekeza klabu hiyo kubaki na wachezaji 13 tu kati ya 25 waliokuwamo kikosini katika msimu uliomalizika.
Katika ripoti yake, Logarusic aliutaka uongozi kusajili kipa mwenye uwezo unaokaribiana na kipa wake, Ivo Mapunda au kumzidi ili kumwongezea hali ya ushindani langoni, ndiyo maana Bathez anayetajwa kuchukua nafasi hiyo baada ya kumaliza mkataba wake na Yanga.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Pope,  alikiri wapo kwenye hatua za awali kabisa za mazungumzo na baadhi wa wachezaji akiwamo Saad Kipanga wa Mbeya City, Edward Charles wa JKT Ruvu pamoja na wengine waliopendekezwa na Mkurugunzi wa Ufundi, Moses Basena.
"Kocha alipendekeza tusalie na wachezaji 13 pekee katika kikosi cha sasa, itatulazimu kusajili wachezaji 12 ili kufikisha idadi ya wachezaji 25 wanaotakiwa, bado tupo kwenye hatua za awali na baada ya muda mfupi tutatoa taarifa ya kuwa ni mchezaji yupi tumemsajili ila kwa sasa ni mapema sana kusema," alisema Hans Pope.
"Ni kweli tumekuwa na mazungumzo na baadhi ya wachezaji wa timu za Ligi Kuu, lakini bado hatujafikia muafaka wowote, napenda kusisitiza kuwa hayo ni mazungumzo tu na bado yako kwenye hatua za awali  kabisa."
Akizungumzia mapendekezo yaliyotolewa na Logarusic juu ya kuachana na idadi hiyo kubwa ya wachezaji, Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema: "Hatuwezi kuwatema wachezaji moja kwa moja, tutakaa chini na kuangalia ni kipi cha kufanya kwani wameisaidia timu kwa kiwango fulani, haijalishi kama mchezaji amemaliza mkataba na sisi pia tutaangalia cha kufanya, hili tutalifanya baadaye siyo sasa."
Hans Pope alisema pamoja na wachezaji wengine watakaowasajili watashusha mabeki wawili wa pembeni wa maana sana kwa wakati mmoja huku pia kiungo mmoja wa ukabaji na mshambuliaji nao wanasakwa.
"Washambuliaji wanaotakiwa ni wawili tena wenye uchu wa kutikisa nyavu na makipa wawili," alisema Kamwaga.
"Washambuliaji tunataka kuanza kuangalia hapa ndani, majina tunayo lakini hatuwezi kuyatamka sasa."

No comments: