BEKI wa kimataifa wa Simba, Joseph Owino,
amemtaka wazi kuwa anatafuta nafasi ya kucheza soka la kulipwa barani
Ulaya na tayari klabu ya IB Vestmannaeyjar (IBV) ya Iceland anayocheza
kipa wa zamani wa Simba, Abel Dhaira, imedhamiria kumchukua.
Owino ambaye ni raia wa Uganda, ameiambia
Mwanaspoti kwa njia ya simu akiwa kwao akisema: "Nafikiri sasa ni muda
mzuri wa kucheza soka la kulipwa Ulaya, nimekuwa na msimu mzuri nikiwa
Simba, sasa naangalia mbele.
"Kiukweli kuna klabu imeonesha nia ya kunisajili
na hii ni ile anayocheza rafiki yangu Dhaira, nafikiri wameshaona
ninavyocheza na kilichobaki sasa ni hao kufanya mazungumzo na Simba.
"Naelewa kuwa nina mkataba na Simba na hivyo
ninaomba iwapo Simba watafuatwa na klabu yoyote kwa ajili yangu wasisite
kuwa radhi na pia wasiache kunishirikisha kwenye suala hilo."
Naye kocha wa IBV, Ragnar Eyjolfson, ameliambia
Mwanaspoti kupitia mtandao wa kijamii wa 'Skype' akisema: "Ninamjua
Owino, nilishawahi kutambulishwa kwake na Dhaira kipindi nilipoenda
Uganda mwaka 2012.
"Nilizungumza naye kuhusu kucheza soka kwenye
klabu yetu, ilikuwa mwaka 2012. Lakini kwa sasa siwezi kusema lolote,
kama litakuwapo basi litawekwa wazi."
Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema:
"Hatujapokea taarifa zozote kuhusu Owino kuhitajika na timu ya Ulaya,
lakini kama timu inamhitaji inaruhusiwa kuja, tutazungumza kwa kuwa bado
ana mkataba na Simba."
Dhaira naye alisema: "Ni kweli Owino ana
mawasiliano na baadhi ya viongozi wa timu hii tangu siku nyingi, lakini
sijajua iwapo amefanya mambo yanayohusu yeye kuhamia huku."
No comments:
Post a Comment