YANGA imepanga kumsainisha rasmi mkataba kiraka Mbuyu Twite lakini imetegesha rada zake Cameroon kupata straika la maana
kuziba nafasi ya Didier Kavumbagu aliyechepukia Azam FC.
Akizungumza na Mwanaspoti Kaimu Mwenyekiti wa
Kamati ya Usajili ya Yanga,Mussa Katabaro alisema tayari wameshapokea
ripoti ya kocha wa Hans Pluijm ambaye ametaka kusakwa kwa nguvu zote
mshambuliaji mpya akiwa na sifa mbili kubwa.
Katabaro alisema wanataka straika mwenye uwezo
katika kufunga kwa kutumia miguu pamoja na vichwa kitu ambacho kilikuwa
kinapungua kwa Mrundi Kavumbagu.
Alisema katika mchakato huo tayari rada zao zipo
Afrika Magharibi hususani Cameroon ambapo kuna jina moja limefika mezani
kwao na kazi imeshaanza kulimulika.
"Tunataka kufanya usajili wenye akili, hatutaki
kukurupuka katika hilo, tunakutana mwisho wa wiki hii kufuatilia mambo
fulani ya wapi tutampata mtu muafaka atakayetusahaulisha Kavumbagu
haraka na wapo wengi kwa mujibu wa kocha wetu (Pluijm)," alisema
Katabaro.
"Tumeanza kazi hiyo taratibu sio kwamba hatujaanza
kabisa, kuna nchi kama Senegal na Cameroon ambako tumehakikishiwa na
tunajipanga, tupeni muda tuisuke Yanga,"alisisitiza. Yanga haijatoa
orodha kamili ya wachezaji inaowapukutisha ingawa kamati ya usajili
imeweka bayana kwamba hakutakuwa na majina mengi makubwa.
No comments:
Post a Comment