HALMASHAURI ya Wilaya ya Moshi inaandaa mpango wa kuboresha soko la
Mwika, ili liwe la kisasa na kuondoa athari za ajali katika eneo hilo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI), Agrey Mwanri, alieleza hayo jana wakati akijibu swali
la Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP), aliyetaka kujua mpango wa
serikali wa kutafuta eneo kubwa na kuhamisha soko la Mwika kwa kuwa
lipo barabarani, hivyo kuna hatari ya wananchi kugongwa na magari.
Akiendelea kujibu swali hilo, Mwanri alisema halmashauri hiyo
imepanga kukopa fedha katika Bodi ya Mikopo katika serikali za mitaa,
ili kutekeleza mpango huo.
Alisema kwa sasa halmashauri hiyo ipo katika hatua za upembuzi
yakinifu wa eneo hilo ili kujua gharama zitakazohitajika kukamilisha
kazi hiyo.
“Wakati mpango wa muda mrefu wa kuboresha soko hilo unaendelea,
halmashauri imewasilisha maombi kwa Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa
wa Kilimanjaro ili iweze kuruhusu ziwekwe alama za tahadhari kwa maana
ya kuonyesha maeneo ya kuvukia katika eneo hilo,” alisema Mwanri.
Alitoa wito kwa wananchi kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zisizo za lazima.
Pia aliwataka wafanyabiashara kutumia maeneo yaliyotengwa kwa ajili
ya biashara na kuacha kuweka bidhaa barabarani kwa ajili ya usalama wa
mali zao.
No comments:
Post a Comment