Thursday, 8 May 2014

KKKT watoa tamko Kanisa la Mwanza

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria (DMZV), limeitaka Serikali kuhakikisha inawatafuta watu waliohusika na tukio la bomu lililolipuka kanisani hapo juzi.
Pia, limewataka Wakristo kuwa watulivu, wasiogope wala wasitishwe na mashambulizi hayo na kwamba wasilipize kisasi.
Akizungumza kwenye Kanisa la Imani Makongoro Misheni jana, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki Ziwa Victoria, Andrew Gulle alisema wanaamini shambulio hilo ni la kigaidi na kwamba, Serikali inapaswa kuchukua hatua ya kuwasaka wanaohusika.
“Kanisa tunaamini tukio hili linahusiana na ugaidi, umefika wakati Serikali ikachukua hatua za kuwasaka waliohusika ili sheria ifuate mkondo wake,” alisema Gulle.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya dini wanasema huenda tukio hilo linatokana na migogoro inayoendelea kanisani hapo kwa sababu tayari kuna baadhi ya waumini wamejitenga kwa kuanzisha kanisa lingine.
“Wasikwepe matatizo yao ya ndani, kuna askofu aliuawa kwa kupigwa tofali kutokana na migogoro, hivyo hata hili (tukio) litakuwa ni migogoro inayoendelea,” alisema mmoja wa waumini ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Askofu Gulle alikanusha kuwapo kwa migogoro kanisani hapo na kwamba, tukio hilo halihusiani na mgogoro wowote ndani ya Kanisa bali ni ugaidi.
Majeruhi aendelea vizuri
Hali ya majeruhi wa mlipuko wa bomu uliotokea kanisani hapo, Benadeta Alfred, imeelezwa kuendelea vizuri katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando alikolazwa. “Hali ya mgonjwa ni nzuri ukilinganisha na tulivyompokea kwani hata kuongea alikuwa hawezi, lakini hivi sasa anaweza kuongea japo kwa shida,” alisema Lema.

No comments: