Sunday, 4 May 2014

Simba yagoma kumuuza Tambwe Yanga

SIMBA imeapa kwamba hata kwa dau la kiasi gani,Amissi Tambwe na Jonas Mkude hawauzwi kwa
klabu yoyote ya Tanzania. Hivyo wasijisumbue.
Kauli hiyo ya Simba imekuja baada ya Azam FC kuwasajili Didier Kavumbagu na Frank Domayo wa Yanga ambao walikuwa wachezaji huru.
Klabu hiyo pia ilihusishwa na mipango ya kuwasajili Tambwe na Mkude ili kuimarisha kikosi chake tayari kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema; “Tambwe na Mkude bado ni wachezaji wetu na hatuwauzi kwa klabu yoyote hivi sasa. Kama kuna timu inawahitaji wajue hawapati kitu na hatuna muda wa kuzungumza nao kwani hawa ni wachezaji wetu na tunahitaji mchango wao katika timu.”
“Tunaweza kuwauza pengine nje ya nchi tena kwa dau kubwa, kwa maana hatuwezi kukataa ofa nzuri kutoka nje ya nchi bila sababu huko tunaweza kuwauza lakini siyo kwa klabu za humu ndani.”
Kamwaga alisema hawawezi kuwauza nyota hao kwa klabu wanazoshindana nazo kwavile wanajua na wameona madhara yake. Hivyo kama kuna timu ilipanga kuwasajili iandike maumivu. “Kila mchezaji ana bei yake hapo, Tambwe na Mkude tunaweza kuwauza nje ya nchi tena kwa dau kubwa, lakini siyo Tanzania tena kwa timu tunazoshindana nazo.”
Tambwe amebakiza mwaka mmoja wa mkataba wake kama ilivyo kwa Mkude na ndiyo wachezaji wanaoibeba Simba katika mechi mbalimbali za klabu hiyo.

No comments: