TIMU ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ‘Ngorongoro
Heroes’ juzi Jumapili ilivuka hatua ya awali ya mechi za kufuzu Kombe la
Mataifa ya Afrika kwa vijana lakini timu hiyo haikubahatika kufunga bao
hata la kuotea kwenye mechi mbili ilizocheza na Kenya.
Ngorongoro Heroes na Kenya zilitoka suluhu mjini
Nairobi wiki chache zilizopita kabla ya kutoka sare ya aina hiyo hiyo
kwenye mechi ya marudiano Jijini Dar es Salam. Ngorongoro ilishinda kwa
penati 4-3 na kufuzu kwenye hatua inayofuata na ratiba inaonyesha kuwa
itavaana na Nigeria katika hatua hiyo ya pili.
Akizungumzia ubutu unaoikabili timu hiyo, Kocha
John Simkoko aliliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuitafutia timu
hiyo mechi nyingi za kirafiki ili iweze kujiandaa vizuri kabla ya mechi
ya marudiano na kuwatengenezea vijana hao hali ya kujiamini pindi
wanapofika kwenye eneo la hatari la timu pinzani na kuweza kufunga.
Kwa upande wake, Kocha wa zamani wa Azam FC,
Stewart Hall aliyekwepo pia kwenye benchi la Ngorongoro Heroes alisema
kuwa tatizo la ushambuliaji limekua sugu hapa nchini hivyo kuwataka
waalimu na wakufunzi wa michezo kuanzisha program mbalimbali
zitakazosaidia kutatua tatizo hilo.
“Ushambuliaji ni tatizo kubwa katika medani ya
soka hususani hapa nchini Tanzania, ni vyema walimu wakalitazama hili
kwa jicho la pili ili kuweza kulitatua,” alisema Hall anayefanya kazi
kwenye Mradi wa Symbion unaohusika zaidi na soka la vijana hapa nchini
chini ya usimamizi wa klabu ya Sunderland inayoshiriki ligi kuu ya
Uingereza.
No comments:
Post a Comment