Friday, 2 May 2014

Niyonzima asimulia makubwa Yanga

Niyonzima akiwa katika pozi ya picha na familia yake jijini Dar es Salaam.
KIUNGO wa Yanga, Mnyarwanda Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ alipotea ghafla kwenye timu na kusababisha kila mtu azungumze anachokijua juu ya tukio hilo.
Wapo waliodai amejiondoa mwenyewe kikosini makusudi ili kuficha aibu kwa sababu kiwango chake kimeshuka, wengine walidai ana matatizo na benchi la ufundi chini ya kocha Mholanzi, Hans Van Pluijm.
Ndipo Ukombozi, ikaamua kumtilia miguu ili kujionea na kuzungumza naye kwa undani juu ya suala hilo. Ilikuwa nyakati za jioni nyumbani kwa mchezaji huyo ambaye anaishi Magomeni, Makuti jijini Dar es Salaam.
Hapo anakaa pamoja na familia yake; mkewe anayeitwa, Naillah ambaye ni Mnyarwanda mwenzake, mtoto wao wa kiume , Ramsey, kaka zake, Hamduni na Prezo na ndugu na jamaa wengine.
“Nimepata matatizo makubwa kwenye kipindi hiki kwa sababu haijawahi kunitokea na kwangu naona mapya,” anasema Niyonzima baba wa watoto wawili binti mmoja, Halila (9) na Ramsey (5).
“Watu wanazungumza tu, unajua anaweza kuibuka mtu mwenye nia mbaya akatunga yake ilimradi kumharibia mtu. Ukweli kamili ni kwamba, nilikuwa mgonjwa. Nimeumwa sana malaria na baadaye walikuja kunigundua na homa ya matumbo.
“Kwa anayekumbuka nilipokuwa Misri kwenye mechi ya marudiano na Al Ahly muda mchache kabla ya kuanza, niliondolewa kikosini kwa sababu ya malaria, nikashindwa kucheza.
“Nilitumia dawa, tukarudi Dar es Salaam baadaye nikapata nafuu na kuanza mazoezi na wenzangu hata ile mechi na Mgambo JKT niliingia kipindi cha pili kumpokea Ngassa (Mrisho). Lakini baadaye, niliumwa sana na baada ya vipimo niligundulika na homa ya matumbo pamoja na malaria kali,”anasema Niyonzima.
“Siku hiyo nilikuwa nyumbani ndipo nikazidiwa na kukimbizwa hospitali ambako daktari aliamua nipumzishwe kwa kulazwa ilikuwa ngumu kujiuguza nikiwa nyumbani (anaitaja hospitali hiyo inaitwa Nikwezi ipo Magomeni).
“Wakati huo mechi za ligi zilikuwa zinaendelea hadi kuja kupata nafuu, zilikuwa zimesalia mechi mbili tu na hapo nilikuwa sina nguvu na uchovu wa ugonjwa, sikuwa fiti kwa ujumla, nikaamua nijitibie hadi nipone kabisa.
“Lakini nilichokuja kukisikia baadaye hakika siamini kwangu naona ni makubwa, nasumbuliwa sana ndugu na jamaa wakitaka kujua kilichonikuta. Simu nyingi zinapigwa kutoka nyumbani Rwanda kuwa nimeondolewa Yanga ndiyo maana sichezi, wakati siyo kweli,” anafafanua Niyonzima.
“Kusema ukweli, kitendo hicho kimenisikitisha sana, watu hawajui utu, mimi ni mchezaji mkubwa, hata siku moja siwezi kuogopa mechi, nimekaa Yanga na kupitia vipindi tofauti vigumu na raha. Tulifungwa na Simba bao 5-0 mbona sikukimbia ijekuwa hizi mechi za kawaida kwa mchezo upi?

“Wajue nimetoka Rwanda na kuja Tanzania kwa ajili ya kucheza na siyo kukaa.Juu ya kiwango, mbona kuna kipindi nilikuwa siko vizuri na nilisema ukweli kuwa siko fiti,ninachosema, watu waliozusha hayo walidhamiria kunichafua, lakini sitawapa nafasi washinde.
“Badala yake, nitapambana kwa nguvu zote hadi mwisho, bila kukata tamaa kuhakikisha nafanikiwa. Moyoni inaniuma kwa sababu mimi ni binadamu, lakini mwisho wake upo, hata hivyo nashukuru sana kwa sababu nimejifunza kitu juu ya maisha haya.”
Ugomvi na benchi la ufundi
“Sina matatizo na benchi la ufundi, kocha wangu, Pluijm pamoja na wengine, sina matatizo na uongozi wangu na wote wanajua kuwa nilikuwa naumwa,” anasema.
Mwandishi wetu alizungumza na Pluijm aliyesema: “Ninachojua, Niyonzima alikuwa anaumwa ndiyo sababu hatukuwa naye kwenye mechi za mwishoni, sina tatizo naye hata kidogo.”
Kocha msaidizi, Boniface Mkwasa anasema: “Yaani hata mimi nashangaa, nayasikia tu yanazungumzwa mitaani, lakini ninachokijua, Niyonzima alikuwa hayupo kwenye timu kwa sababu alikuwa mgonjwa.”
Kuhusu maneno yanayozungumzwa kama anavunjiwa mkataba, Mkwasa alisema: “Niyonzima ni mchezaji wetu na tunamuhitaji kwenye timu, sasa hayo yanayozungumzwa sijui yanatoka wapi.” Kwa upande wa Niyonzima juu ya suala hilo, alisema: “Sijui lolote juu ya hilo, nafikiri mimi ndiyo mhusika, kama kuna lolote ningejua na ningekwambia.”
Familia yake
Mkewe Naillah anasema: “Nimesikitishwa na kushangazwa juu ya hayo, mwenyewe nimekuwa nasumbuliwa sana na simu kutoka nyumbani wakitaka kujua yanayojiri juu ya Haruna (Niyonzima).
“Mimi ndiyo nakaa naye, chochote nitajua jamani mume wangu alikuwa anaumwa.”
Mdogo wake Niyonzima ambaye amekuja kumtembelea kutoka kwao Rwanda anasema: “Nimeshangaa na yanayozungumzwa na hasa simu ninazopigiwa kutoka nyumbani Rwanda kuwa wamesikia kwenye vyombo vya habari Niyonzima ameondolewa Yanga na kila unapowaeleza wanajua tunawadanganya.”

No comments: