“Nilitaka kujiua kwa njia yoyote ambayo ningeona inafaa, lakini
nilirudisha moyo nyuma kwa sababu ingekuwa shida kubwa nyumbani.”
Hayo ni maneno ya aliyekuwa Miss Tanzania 2014,
Sitti Mtemvu aliyeamua kulitema taji hilo la ulimbwende baada ya
kubebeshwa kashfa za udanganyifu wa umri wakati akishiriki mashindano
hayo.
Aliongeza: “Sikuwa na amani, niliishi maisha ya
hofu, kujifungia ndani, kulia wakati wote. Ilifikia hatua baba yangu
alipata mshktuko kiasi cha kwenda kutibiwa Afrika Kusini. Mama yangu pia
alipata mshtuko...ningeweza kumpoteza.”
Anazikumbuka siku 30 za majonzi na maumivu, ambazo
kwa kiasi kikubwa zilimuathiri mama yake mzazi ambaye ndoto za binti
yake kwenye mashindano ya urembo zilifika tamati.
“Mama yangu alisali na mimi, alinipigania,
hakuonyesha hadharani jinsi gani anaumia, lakini ukweli ni kwamba
nilimwona alivyokuwa anadhoofu na kukosa raha. Nyumba yetu iligeuka
sehemu ya huzuni, amani ilitoweka ni kama tulikuwa na msiba.”
Sitti anasema siku moja mama yake alimwambia:
“Sitti mwanangu, nilipompoteza mama yangu nililia na kuumia sana, lakini
machungu ninayoyasikia sasa na utu uzima wangu ni mazito.”
“Sikutamani kumwona mama yangu analia, iliniuma na
hata sasa nawaza machungu na maumivu aliyopitia kwa ajili yangu,”
anasema na kuongeza: “Asichokijua mama, siku moja nilikuwa natoka
chumbani kwangu nikimwangalia mama akiwa na gazeti lililokuwa na habari
yangu. Nilishikwa na uchungu na kurudi chumbani, niliona kama vile dunia
imeniangukia.”
“Wakati huo wote baba yangu alivumilia bila
kuonyesha maumivu yake, daima alikuwa mtulivu na japo alipinga vikali
mimi kushiriki Miss Tanzania,” anasema Sitti.
Baba aliniambia: “Mwanangu usijali, hivi siyo vita vyako tena, sidhani kama sasa wanakutafuta wewe tena, utabaki kuwa mwanangu.”
Anasema kuna wakati baba yake alikwenda Afrika
Kusini na akiwa huko alimtumia ujumbe wa kumuomba msamaha na alimwambia
kwamba hizo ni changamoto.
“Aliniambia yeye alikuwa na wasiwasi na mimi,
lakini kwa upande wake yupo vizuri, hajawahi kuandikwa sana, lakini kama
mzazi ilimuuma sana.”
Sitti anasema alikuwa katika wakati mgumu kiasi cha kufikia uamuzi wa kutupa laini yake ya simu ya zamani.
“Wakati huo nilikuwa sisomi sana magazeti, nilikuwa naingia
kwenye blogu na mitandao. Kwenye Instagram nilishuhudia vikiandikwa vitu
ambavyo sivijui kabisa,” anasema.
“Marafiki walijitenga na mimi, nadhani sababu ilikuwa ni kunipa muda wa kufanya uamuzi kwa yale yaliyokuwa yakiniandama.
“Wakati mwingine nilikuwa najikuta ninalia, halafu
ninacheka yaani ni maumivu makali ambayo sikuwahi kuyafikiria, siku
zilikuwa zinatofautiana.”
Sitti anasema suala hilo japokuwa lilikuwa baya
kwa upande wa baba yake ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Temeke, lakini
anahisi lilimjenga kisiasa.
“Katika mambo ya siasa, suala langu limempa mwanga baba ingawa kuna watu walitegemea angeporomoka,” anasema.
Ili kuepuka kushambuliwa kwenye mitandao, Sitti anasema aliamua kujiondoa kwenye mitandao yote kwa miezi kadhaa.
“Nilijitoa kwenye Facebook, Instagram, Twitter na
katika mitandao mingine tangu Mei mwaka jana, maana nilifikia hatua
nikajiona kama napata adhabu.”
Sitti anasema baada ya yote hayo, anaami ipo siku
mambo yatakwenda sawa na atakuwa na mchango wa kuielimisha jamii kuondoa
dhana na mitazamo isiyokuwa na ukweli kupitia mitandao.
Hata hivyo, anasema siyo sahihi kuweka maisha ya
faragha ya mtu mitandaoni bali ni vyema kutumia namna nyingine ya
kufikisha taarifa hizo.
Alipoulizwa kama anafahamu ni nani aliyetoa
nyaraka zake za vyeti vya kuzaliwa, pasi ya kusafiria, leseni ya udereva
Sitti alisema hadi leo hafahamu.
Licha ya hekaheka aliyoipata mrembo huyo aliyetoka Kanda ya Temeke, anasema familia yake ndiyo iliyoathirika zaidi.
No comments:
Post a Comment