Thursday, 1 May 2014

Baba amuua mwanaye kwa kumkata na kisu shingoni

MKAZI wa Kitongoji cha Mrama Kijiji cha Musimi Kata ya Sepuka, Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Joseph Benjamin (61), amemuua mwanaye, Joramu Joseph (36) kwa kumpiga kisu shingoni, usiku akiwa nyumbani kwake wakati wakiwa wamelewa pombe.
Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP Thobius Sedoyeka alisema, tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki, saa 1:00 usiku katika Kijiji cha Musimi.
Aidha, Kamanda Sedoyeka alisema baba mzazi Joseph Benjamin akiwa nyumbani kwake usiku alimchoma kisu shingoni na begani upande wa kushoto hadi kufa.
Uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa, chanzo cha tukio hilo ni ulevi wa pombe na kutokana na ulevi huo marehemu alimtukana baba yake matusi makubwa ya nguoni kitendo ambacho kilimchukiza na kusababisha mtuhumiwa kufanya kitendo hicho cha kumchoma kisu shingoni kwa hasira.
"Baada ya mauaji hayo kufanyika mtuhumiwa Joseph Benjamin alijisalimisha mwenyewe katika kituo kidogo cha Polisi cha Sepuka na baadaye akapelekwa kituo kikubwa cha polisi Ikungi," alisema.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi linawaasa wananchi kupunguza ulevi ambao umekuwa ni chanzo cha vitendo vya kikatili na upotevu wa amani katika maeneo yetu na nchi kwa ujumla.

No comments: