NI mwisho wa zamani. Hakuna marefu yasiyo na mwisho. Juzi
Jumapili inaweza kuwa siku ya mwisho kwa beki wa kushoto wa Chelsea,
Ashley Cole, kuvaa jezi katika Uwanja wa Stamford Bridge baada ya nyota
huyo kuondoka uwanjani hapo akiwa analia.
Cole, 33, alimwaga machozi wakati akiwaaga
mashabiki wa Chelsea baada ya pambano la mwisho la Chelsea uwanjani
Stamford Bridge dhidi ya Norwich City katika msimu huu wa Ligi Kuu
England, mechi hiyo ilimalizika kwa timu hizo kutofungana.
Wiki ijayo Chelsea itacheza mechi ya mwisho ya
msimu dhidi ya Cardiff City lakini itakuwa ugenini. Baada ya mechi dhidi
ya Norwich, wachezaji wa Chelsea walizunguka uwanja wakiwaaga mashabiki
wao na ndipo Cole alipoangua kilio kwa uchungu.
Baadaye beki huyo alibembelezwa na nyota wengine
wawili wa Chelsea, Frank Lampard na John Terry, ambao nao hawana uhakika
wa kuendelea kuwepo katika kikosi cha Chelsea msimu ujao baada ya
kupoteza namba.
Cole amepoteza nafasi yake Chelsea baada ya
kuporwa namba na Mhispaniola, Cesar Azpilicueta, ambaye licha ya kuanzia
maisha yake katika upande wa kulia, alihamishiwa upande wa kushoto na
kocha, Jose Mourinho na amekuwa akifanya vyema.
Cole mkataba wake utamalizika mwishoni mwa msimu
huu na atakuwa huru kujiunga na timu yoyote anayotaka baada ya Chelsea
kushindwa kumpatia mkataba mwingine.
Cole alijiunga Chelsea mwaka 2006 katika uhamisho
uliokuwa na utata mkubwa, tangu hapo ameichezea Chelsea zaidi ya mechi
200 kwa mafanikio akitwaa ubingwa wa Ulaya, ubingwa wa Europa, mataji
manne ya Kombe la FA na mawili ya Ligi Kuu England.
Kumekuwapo na uvumi kwamba nyota huyo amekuwa
anatakiwa na Real Madrid ya Hispania huku pia akihusishwa kucheza katika
Ligi Kuu Marekani ambako inadaiwa klabu ya New York Bulls inamhitaji.
Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers, pia anadaiwa
kumtaka beki huyo wa zamani wa Arsenal wakati huu upande wa kushoto wa
timu hiyo ya Anfield ukiwa unalegalega tangu kuumia kwa Jose Enrique.
No comments:
Post a Comment